Watanzania nchini wametakiwa kuachana na fikra potofu za kuamini kuwa
ugionjwa wa fistula kwa wanawake unasababishwa na kuwa na mahusiano ya
kingono na wanaume wengi ama kulogwa kwani ugonjwa huo unasababishwa na
kuchwelewa kwa mama mjamzito kujifungua hivyo kusababisha tundu ambalo
humletea athari za kiafya.
Mratibu wa Shirika lisilokuwa la kiserikali la Maternity Afrika, Paulo
Letura ,Amesema kuwa ugonjwa huo unasababishwa na umbali mrefu wa vituo vya
afya kwa kina mama wajawazito hivyo amewataka kina mama kuwahi katika vituo
vya afya na kujifungua katika vituo hivyo badala ya kwenda kwa wakunga wa
jadi.
Paulo Letura amesema kuwa kwa sasa wanafanya juhudi za kutoa elimu hasa
maeneo ya vijijini ambako uelewa ni mdogo na kuwataka wajawazito wafike
mapema kwenye vituo vya afya kwa kuchelewa kunasababisha msuguano wa mtoto
tumboni ambao husababisha tundu karibu na kibofu cha mkojo na karibu na
utumbo mkubwa.
Letura alisema hayo jana wakati wakitoa masaada wa kitaalamu wa matibabu na
upasuaji kwa kina mama pamoja na kutoa misaada ya kibinadamu.
Mkurugenzi wa shirika hilo ambaye ni Daktari aliyebobea katika ugonjwa huo
Dr.Andrew Browing anasema kuwa wamekua wakifanya kazi na vituo mbalimbali
vya afya ikiwemo KCMC,CCBRT katika kuhakikisha kuwa wakinamama wanapata
tiba ya ugonjwa huo hivyo amewashauri kinamama wajitokeze kupata matibabu
badala ya kukaa nyumbani.
Kwa upande wake Mtaalamu wa Afya katika shirika hilo Paivi Karlssom
amewataka kina mama kujenga utamaduni wa kujifungulia katika vituo vya afya
ili wapate msaada wa kitaalamu badala kujifungulia kwa wakunga wa jadi.
Kwa mujibu wa takwimu za shirika la afya duniani (WHO) Wanawake na
wasichana 3000 wanapata tatizo hili wenye umri kati ya miaka 22 hadi 24
hupatwa na tatizo hili zaidi.