Wananchi wa kijiji cha Kambi ya Simba kilichopo wilaya ya Karatu
mkoani Arusha wanakabiliwa na changamoto ya ukosefu wa huduma za afya
hali inayowalazimu kutembea umbali wa kilomita 40 kufuata huduma hiyo
muhimu.
Aidha wamekuwa wakikumbwa na adha kubwa hasa kwa kina mama wajawazito
wanapokwenda kujifungua hali iliyowapelekea wananchi hao
kuunganisha nguvu na kujenga kituo cha afya kitakachowasogezea huduma
za afya Karibu.
Mwenyekiti wa Kijiji hicho akisoma taaarifa ya utekelezaji wa mradi
huo mbele ya Uongozi wa Kampuni ya bia ya TBL iliyofika kijijini hapo
na kutoa msaada wa vifaa tiba vyenye gharama ya shilingi milioni 22
ili kusaidia wodi ya uzazi na watoto ikiwa ni njia mojawapo ya kuunga
mkono shughuli za kijamii.
Amesema kuwa baada ya kukabiliwa na changamoto hiyo kwa muda mrefu
wananchi waliamua kujenga kituo chicho cha afya kwa kushirikiana na
Mamlaka ya Ngorongoro na kwa sasa wako katika umaliziaji wa nyumba za
wauguzi pamoja na kuweka vifaa mbali mbali hivyo ameishukuru TBL kwa
msaada huo.
Mkurugenzi Mtendaji wa Kampuni ya Bia ya TBL ,Robin Goetzsche na
Afisa Mahusiano Doris Malulu wamesema kuwa wameguswa kuisaidia jamii
hiyo kutokana na mwamko wao wa kulima shahiri na kuonyesha nia ya
kutumia fedha wanazozipata kujiletea maendeleo hivyo kuwa mfano wa
kuigwa kwa wakulima wote wa Shahiri nchini kote.
Wananchi wa Kijiji cha Kambi ya Simba huishi kwa kutegemea kilimo cha
shayiri ambayo wanaiuza kwa kampuni ya TBL na kujipatia kipato
kinachowawezesha kufanya shughuli mbalimbali za maendeleo.