Mkurugenzi wa kupunguza umaskini kutoka Wizara ya
Fedha, Ana Mwasha (kulia) akifungua kongamano, linalojadili yaliyojiri
katika Malengo ya Millenia na nini kinastahili kufanywa katika SDG's ili
kuhakikisha mafanikio katika ukumbi wa mikutano wa Taasisi ya Uchumi na
Utafiti wa Kijamii nchini (ESRF). Kushoto ni Kaimu Mkurugenzi wa Taasisi
ya Uchumi na Utafiti wa Kijamii nchini (ESRF) Dk.Oswald Mashindano na
Katikati ni Naibu Mkurugenzi Mkazi wa Shirika la Maendeleo la Umoja wa
Mataifa (UNDP)- Programme, Amon Manyama.(Picha na Zainul Mzige wa modewjiblog)
Na
Mwandishi Wetu
MKURUGENZI wa Kupunguza Umasikini kutoka Wizara ya Fedha, Anna Mwasha
amesema changamoto za uwezo wa kifedha kutekeleza miradi mbalimbali
iliyokuwa katika Malengo ya Milennia, zinatoa ishara tosha ya kubadili
mikakati ili kuwa na mafanikio katika Mipango ijayo ya Maendeleo Endelevu
(SDGs)
Alitoa
kauli hiyo jana wakati akizungumza na washiriki wa kongamano, linalojadili
yaliyojiri katika Malengo ya Millenia na nini kinastahili kufanywa katika
SDGs ili kuhakikisha mafanikio.
Alisema ipo haja ya kuimarisha makusanyo ya fedha za ndani na kuacha
kutegemea wahisani, kwa kuwa moja ya sababu za kushindwa kutekelezwa kwa
Malengo ya Millenia ni ahadi za wahisani kutotekelezwa.
Alisema kipengele cha nane katika Malengo ya Millennia,
kiligusia ushirikiano wa kimataifa, ahadi ambazo amesema ukiachia nchi za
Luxemburg, Denmark, Sweden na Norway, mataifa mengi hayakutoa asilimia 0.7
ya pato lao la ndani, ambalo lilikubalika kimataifa kusaidia Malengo ya
Millennia kwa nchi masikini.
Alisema ili kuwepo na mafanikio katika miradi mipya na
ile inayoendelezwa kutoka MDGs, iko haja ya kuangalia jamii iliyopo
vijijini, ambako ndiko kwenye umasikini wa kutisha, ingawa Tanzania
imefanya vyema kuondokana na umasikini wa chakula.
Umasikini wa chakula umepungua hadi asilimia 9 wakati
Malengo ya Millenia yalikuwa ni asilimia 11.
Alisema ipo haja ya kufungua mawasiliano ya vijijini,
kuinua kilimo, kuwapatia nafasi ya masoko na kuinua huduma za
jamii.
Pamoja
na kuzungumzia uwezo wa kifedha, alisisitiza haja ya wadau kuangalia namna
ya kushirikisha sekta binafsi katika kutafuta vyanzo vya fedha kwa ajili ya
kutekeleza miradi mbalimbali ili kukabili umasikini.
Naibu Mkurugenzi Mkazi wa Shirika la Maendeleo la Umoja wa Mataifa (UNDP)-
Programme, Amon Manyama akizungumza kwenye kongamano la siku moja
linalojadili yaliyojiri katika Malengo ya Millenia na nini kinastahili
kufanywa katika SDG's ili kuhakikisha mafanikio lililofanyika katika ukumbi
wa mikutano wa Taasisi ya Uchumi na Utafiti wa Kijamii nchini
(ESRF).
Alisema mahitaji ya msingi katika kupunguza umasikini,
hayajafikiwa kwani tumefikia asilimia 28.2 wakati tulitakiwa kuwa asilimia
19.
Alisema ipo haja kubwa ya kuangalia utekelezaji wa
malengo endelevu kwa kuoanisha na mikakati mingine ya kidunia na ya
kikanda, huku kazi kubwa ikiwa kuhakikisha malengo yote 17 yanatekelezwa
katika muda uliopangwa.
Katika kongamano hilo, washiriki walipata nafasi ya kumsikia Balozi
Celestine Mushy kutoka Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa,
akichambua jinsi mataifa yalivyofikia SDGs, michakato inayoendelea na namna
ambavyo anafikiri Tanzania inaweza kunufaika na mkakati mzima wa
maendeleo.
Pia
katika majadiliano, washiriki waliozungumzia haja ya kuangalia takwimu kwa
kuoanisha kwani zimekuwa zikitafutwa na kila mtu mpaka hazijulikani nani
yuko sahihi.
Aidha,
walitaka mkakati wa kiviwanda ndio uzingatiwe kwani ndio unaoonesha dira ya
kufanikisha maendeleo ya kitaifa, kikanda na kibara.
Kongamano hilo liliendeshwa na Taasisi ya Utafiti wa
Masuala ya Uchumi (ESRF) kwa ufadhili wa UNDP.
Kaimu Mkurugenzi wa Taasisi ya Uchumi na Utafiti wa
Kijamii nchini (ESRF) Dk.Oswald Mashindano akizungumza kwenye kongamano
hilo.
Pichani juu na chini ni Mkurugenzi wa Idara ya
Ushirikiano wa Kimataifa Wizara ya Mambo ya Nchi za Nje na Ushirikiano Wa
Kimataifa Balozi Celestine Mushy akiwasilisha mada jinsi mataifa
yalivyofikia SDGs, michakato inayoendelea na namna ambavyo Tanzania inaweza
kunufaika na mkakati mzima wa maendeleo.
Dk. Kenneth Mdadila kutoka kitengo cha uchumi Chuo
Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM) akiwasilisha mada kwenye kongamano
hilo.
Sehemu ya washiriki wakifuatilia mada mbalimbali
zilizokuwa zikiwasilishwa kwenye kongamano hilo.
Pichani juu na chini baadhi ya wadau walioshiriki
kwenye kongamano hilo wakichangia mada kwenye kongamano
hilo.