Wananchi wa Wilaya ya
Rorya, Mkoani Mara, wanaoishi Mji mdogo wa Mirerani Wilayani Simanjiro Mkoani
Manyara, wamemuomba Mwenyekiti wa Chadema jimbo la Rorya, Charles Odero agombee
ubunge wa jimbo la Rorya.
Wakizungumza juzi mji mdogo wa
Mirerani, wananchi hao walisema kupitia umoja wao ikiwemo Mara Group wapo
tayari kumuunga mkono Odero kwani ni kijana mwenye maono na uwezo wa kufuatilia
na kutatua matatizo ya jamii.
Thobias Magati alisema atamuunga
mkono Odero kwa kuwahamasisha ndugu zake waliopo Rorya kwani jimbo hilo
liliongozwa na watu wenye ulimu ya kawaida, mwanasheria, profesa na sasa ni
wakati wa mwinjilisti aongoze Rorya.
“Kupitia Odero wale watu
wanaoturudisha nyuma kwa kudai kuwa wanafikiria kwa kutumia tumbo na siyo akili
tutawakomesha, tuendelee kupambana ili sasa hivi wajitambue na siyo kujali
fedha wanazopewa,” alisema Okuku Obata.
Naye, Odero alisema yupo tayari
kugombea ubunge jimbo la Rorya na anaamini uongozi shirikishi kwa kuwa mbele
yao, katikati na nyuma yao kwa kuwalinda kuwasikiliza na kuwaonyesha njia ya
kuwafikisha mbali kwenye maendeleo.
“Jimbo la Rorya lina fursa nyingi
ikiwemo ziwa Victoria, ardhi yenye rutuba na kuwa mpakani na Kenya, hivyo
hatuhitaji mbunge aliyetuna mifuko ila tunahitaji mbunge mwenye maono na upeo
wa kuona mbali,” alisema Odero.
Alisema kutokana na Rorya kukosa
mbunge makini, wananchi wamekosa fursa nyingi za maendeleo ikiwemo shule za
serikali za sekondari zenye kidato cha tano na sita, barabara nzuri, elimu
bora, maji safi na vituo vya afya.
“Tutawakomesha wale wanaodhani
fedha ndiyo inawapa uongozi kwani tuumefanikiwa kufanya vizuri kwenye uchaguzi
wa serikali za mitaa mwaka jana hivyo tutashinda ubunge na kupata madiwani
wengi zaidi yao,” alisema Odero.
Post a Comment
unashauriwa kutoa maoni muda na wakati wowote na kama unahabari yeyote unaruhusiwa kututumia