ANNAN AONYA WAKENYA KUTOWAPA KURA WATUHUMIWA,MSAKO WA VIGOGO WA MAUAJI YA KIMBARI HAUNA MWISHO
Katibu Mkuu wa zamani wa Umoja
wa Mataifa, Kofi Annan wiki hii amewataka Wakenya kutowapigia kura
wanasiasa wanaokabiliwa na kesi mbele ya Mahakama ya Kimataifa ya Makosa
ya Jinai (ICC), huku maafisa waandamizi wa Taasisi Inayorithi Kazi za
Mahakama za Kimataifa (MICT) wamesema juhudi za kuwasaka watuhumiwa
vigogo watatu wa mauaji ya kimbari zinabakia kuwa kipaumbele cha taaisis
hiyo.
ICC
Annan awaonya Wakenya: Jumanne wiki hii, Katibu Mkuu wa zamani wa
Umoja wa Mataifa, Kofi Annan aliwataka Wakenya kutowapigia kura
wanasiasa wanaokabiliwa na kesi mbele ya Mahakama ya Kimataifa ya Makosa
ya Jinai (ICC).Kenya inatarajia kufanya uchaguzi wake mkuu Machi,
mwakani.Annan ambaye hivi sasa ni mwangalizi wa uchaguzi wa Umoja wa
Afrika (AU) katika uchaguzi huo,alitoa onyo hilo katika ziara yake ya
siku mbili nchini humo. Alisema hadhi ya Kenya inaweza kuharibiwa iwapo
watuhumiwa wa ICC watapigiwa kura. Watuhumiwa hao ni pamoja na Naibu
Waziri Mkuu, Uhuru Kenyatta, anayewania urais na Mbunge, William Ruto
anayepania umakamu wa rais.
ICTR
Mahakama ya Rufaa kuamua kesi ya mwisho kupelekwa Rwanda mwakani:
Jumatano wiki hii, Rais wa Mahakama ya Kimataifa ya Mauaji ya Kimbari ya
Rwanda (ICTR), Jaji Vagn Joensen alitangaza kwamba Mahakama ya Rufaa
itatoa uamuzi hapo mwakani juu ya rufaa ya kupingwa kwa kesi ya
mtuhumiwa wa mauaji ya kimbari,Bernard Munyagishari kwenda kusikilizwa
nchini Rwanda. Akiwasilisha taarifa ya ICTR ya kila miezi sita mbele ya
Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa Jaji Joensen alisema labda kama
umuazi juu ya Munyagishari ukiwa ni kinyume chake, Mahakama ya Rufaa
itakuwa na jukumu la kushughulikia kesi saba zilizobakia mbele yake
ambazo zinatarajiwa kuhitimishwa ifikapo mwishoni mwa 2014.
Vigogo wa mauaji ya kimbari kuendelea kusakwa: Maafisa waandamizi wa
Taaisi Inayorithi Kazi za Mahakama za Kimataifa (MICT) Jumatano walisema
juhudi za kuwasaka watuhumiwa vigogo watatu wa mauaji ya kimbari
zinabakia kuwa kipaumbele cha taaisis hiyo.Rais wa taasisi hiyo, Theodor
Meron alikuwa anahutubia Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa mjini
New York, ambako alitoa wito kwa wanachama wa Umoja huo kusaidia katika
juhudi hizo. Naye Mwendesha Mashitaka wa taasisi hiyo, Hassan Bubacar
Jallow alisema harakati za kuwasaka watuhumiwa vigogo wa mauaji ya
kimbari akiwemo, Felicien Kabuga anayedaiwa kuwa mfadhili wa mauaji
hayo, Waziri wa zamani wa Ulinzi, Augustin Bizimana na Mkuu wa zamani wa
Kikosi cha Walinzi wa Rais, Meja Protais Mpiranya,zimeimarishwa.
Alisema juhudi hizo hazitakoma hadi hapo watuhumiwa hao watakapotiwa
mbaroni na kufikishwa mbele ya vyombo vya sheria.
WIKI IJAYO
Kesi ya Bemba kuendelea kuunguruma wiki ijayo: Kesi ya utetezi
inayomkabili kiongozi wa zamani wa Jamhuri ya Kidemokrasi ya Congo
(DRC), Jean Pierre Bemba anayeshitakiwa kwa uhalifu dhidi ya binadamu na
uhalifu wa kivita itaendelea kusikilizwa Jumatatu ijayo, Desemba 10.
Uhalifu huo unadaiwa kufanywa kati ya mwaka 2002 na 2003 katika Jamhuri
ya Afrika ya Kati.
Mahakama ya Rufaa ICC kuamua juu ya kusikilizwa kwa kesi ya Gbagbo:
Jumatano ijayo, Desemba 12, majaji wa Mahakama ya Rufaa ya ICC, watatoa
uamuzi juu ya rufaa ya kupinga uwezo wa ICC kusikiliza kesi inayomkabili
Rais wa zamani wa Ivory Coast, Laurent Gbagbo.
0 Comments:
Post a Comment
unashauriwa kutoa maoni muda na wakati wowote na kama unahabari yeyote unaruhusiwa kututumia