Na Mwandishi Maalum
Imeelezwa kwamba
Mkataba wa Umoja wa Mataifa wa Sheria ya Bahari ( UNCLOS), Umesaidia sana katika kuifanya dunia kuwa
mahali pa amani, utilivu na salama.
Hayo yamejiri wakati Baraza Kuu la 67 la Umoja wa
Mataifa, lilipoadhimisha miaka 30 ya uzinduzi wa utiaji saini wa mkataba huo,
mkataba ambao katika duru za kimataifa unatambulika kama “ Katiba ya Bahari”.
Uzinduzi wa utiaji saini wa mkataba huo ulifanyika
desemba 10 mwaka 1982 huko Montego Bay,
Jamaica baada ya kukamilika kwa mchakato mgumu wa majadiliano uliodumu kwa miaka 10.
Maadhimisho hayo yamefanyika hapa Umoja wa Mataifa,
ambapo Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa,
Ban Ki Moon,amesema anatiwa moyo na
mwitikio mkubwa ambao umeonyeshwa na jumuiya ya kimataifa katika kuutambua
mkataba huo.
Pamoja na kuridhika huko Ban Ki Moon amezitaka nchi ambazo bado
hazijautambua au kuuridhia kufanya
hivyo, ili hatimaye Mkataba huo
ambao ameutaja kama muhimili muhimu
katika mstakabali wa mataifa na watu wake uweze kutambuliwa na nchi zote.
Hadi kufikia kipindi cha maadhimisho ya miaka 30 tangu kuzinduliwa kwa
mkataba huo mataifa 163 pamoja na Jumuiya ya Ulaya zimekwisha kuuridhia.
Karibu wazugumzaji wote waliozungumza wakati wa maadhimisho hayo walieleza bayana kwamba, kwa
hakika mkataba huo umekuwa nguzo kuu ya
kuwapo kwa hali ya amani na usalama duniani na
kwamba hali ingekuwaje kama
pasingelikuwapo mkataba huo ambao unaanishwa kama moja ya sehemu muhimu katika
sheria za Kimataifa.
Kwa ujumla pamoja na mambo mengine mkataba huo ambao Jamhuri
ya Muungano wa Tanzania ikiwakilishwa wakati huo ,na Waziri Mkuu Mstaafu Mhe, Jaji
Joseph Sinde Warioba, akiwa kiongozi wa ujumbe wa watu watatu ukiwahusisha Balozi Mstaafu Asterius Hyera na Jaji James
Kateka.
Unaratibu na kusimamia kisheria, masuala yote yanayohusu matumizi ya bahari,
ikiwa ni pamoja na usimamizi na matumizi endelevu ya raslimali zinazopatikana
baharini, utunzaji wa mazingira na viumbe hai na utatuzi wa migogoro
inayohusiana na mipaka ya bahari au matumizi ya raslimali hizo.
Akiungana na wazungumzaji zaidi ya 50 waliozungumza
wakati wa maadhimisho hayo, Balozi wa Kudumu wa Tanzania katika Umoja wa Mataifa, Tuvako Manongi, amesema.
“Jamhuri ya
Muungano wa Tanzania ilikuwa miongoni mwa nchi 119 zilizotia saini Sheria ya
Mwisho ya Mkataba wa Sheria ya Bahari.
Mkataba huu ulikuwa kilele cha Sheria muhimu kupitishwa kwa njia ya majadiliano
katika historia ya Umoja wa Mataifa”
Akaongeza kwa kusema “Tanzania inathamini
mchango mkubwa unaotolewa kupitia mkataba huu. Mkataba ambao nchi yangu uliuridhia septemba
30 mwaka 1985 ikiwa ni nchi ya 24 mwanachama wa mkataba. Tunaamini katika umuhimu
wa uwapo wa mkataba na tunafarijika kwa mafaniko ambayo yamekwisha
kupatikana hadi sasa”.
Aidha Balozi
Manongi amesema, Tanzania inatambua vema kwamba katika kipindi cha miaka 30 ya uhai wa Mkataba huo, hapana
shaka kumekuwapo na changamoto nyingi, na kwa sababu hiyo akasisitiza haja na
umuhimu kwa wadau wote kushirikiana
katika kuzikabili changamoto hizo.
Akabainisha pia kuwa yalikuwa ni matumaini ya Tanzania kwamba, kila nchi itawajibika
katika kuhakikisha kwamba bahari inakuwa
mahali salama kwa shughuli za usafiri na
usafirishaji, biashara ya kimataifa, uchimbaji wa mafuta na shughuli nyinginezo
za kiuchumi.
Balozi Manongi
pia amesisitiza umuhimu wa nchi zinazoendelea kusaidiwa na kuwezeshwa ili ziweze kunufaika vema na malengo ya
Mkataba huo, lakini pia katika matumizi
sahihi na endelevu ya raslimali zinazopatikana baharini zikiwamo zile zilizo
nje ya mipaka ya nchi husika na ambazo zinatambuliwa kama urithi wa mwanadamu.
Kama sehemu ya maadhimisho ya mkataba huo, wajumbe waligawia kitabu ambacho
ndani yake kulikuwa na maandiko ya kihistoria kutoka kwa baadhi ya
wajumbe walioshiriki mchakato wa majadiliano yaliyofanikisha kuwapo kwa mkataba huo.
Miongoni mwa
watu mashuhuri waliorejea historia ya ushiriki wao katika mchakato huo, na ambao wametoa maadiko yao kupitia kijitabu
hicho ni pamoja na Mhe, Jaji Joseph Warioba na Jaji James Kateka. Ambapo kupitia maandiko yao wameeleza
hali halisi ya kile walichokabiliana nacho katika kipindi chote cha maandalizi
ya mkataba huo.
Post a Comment
unashauriwa kutoa maoni muda na wakati wowote na kama unahabari yeyote unaruhusiwa kututumia