ICC
Majaji wamwachia huru Ngudjolo: Majaji wa Mahakama ya Kimataifa ya
Makosa ya Jinai (ICC), Jumanne walimwachia huru kwa mashitaka yote
aliyokabiliwa nayo kiongozi wa zamani wa wanamgambo katika Jamhuri ya
Kidemokrasia ya Congo (DRC), Mathieu Ngudjolo. Kiongozi huyo
alishitakiwa kwa makosa ya uhalifu dhidi ya binadamu yaliyodaiwa
kufanyika Mashariki mwa DRC mwaka 2003. Majaji waliamuru mshitakiwa
huyo kuachiwa mara moja na kuitaka ofisi ya Msajili wa Mahakama hiyo
kuchukua hatua zinazofaa za kuwalinda mashahidi.Majaji walisema kwamba
kutokana na ushahidi uliowasilishwa mahakamani, Mahakama imeshindwa
kubaini pasipo mashaka yoyote kwamba mshitakiwa alikuwa kiongozi wa
kundi la wapiganaji la Lendu, lililoshiriki kwenye mapigano katika eneo
la Bogoro, Mashariki mwa DRC, Februari 24, 2003.
Marekani yataka Mudacumura,Ntaganda wakamatwe: Marekani Jumanne
ilitoa wito wa kukamatwa kwa waasi wawili wa Jamhuri ya Kidemokrasia ya
Conmgo (DRC),ikiwa ni pamoja na Sylvestre Mudacumura na Bosco Ntaganda
wanaotakiwa na Mahakama ya Kimataifa ya Makosa ya Jinai (ICC) kwa
tuhuma za uhalifu dhidi ya binadamu na uhalifu wa kivita.Wito huo
umetolewa baada ya ICC kumwachia huru kiongozi wa zamani wa wanamgambo
wa DRC, Mathieu Ngudjolo.Mudacumura ni kamanda wa kundi la waasi la
FDLR ambapo Ntaganda ni kiongozi wa kundi la CNDP.
ICTR
Ban Ki-moon ateua Msajili mpya wa ICTR: Jumatano Katibu Mkuu wa
Umoja wa Mataifa, Ban Ki-moon alimteua Christopher Bongani Majola, kuwa
Msajili mpya ICTR. Raia huyo wa Afrika Kusini ataanza kazi yake rasmi
Januari Mosi, 2013 kwa muda wa miaka minne au hadi hapo ICTR
itakapofungwa.Majola anachukua nafasi iliyoachwa wazi na Adama Dieng
kutoka Senegal, ambaye aliteuliwa na Katibu Mkuu huyo wa UN, kuwa
Mshauri Maalum wa Kuzui Mauaji ya Kimbari tangu Julai 17, 2012.
Waziri wa zamani wa mipango ahukumiwa miaka 35 jela: Mahakama ya
Kimataifa ya Mauaji ya Kimbari ya Rwanda(ICTR) imemhukumu kifungo cha
mika 35 jela Waziri wa zamani wa Mipango wa Rwanda,Augustin
Ngirabatwara baada ya kumtia hatiani kwa mashitaka matatu ya mauaji ya
kimbari.Mahakama iliyokuwa inaongozwa na Jaji William Sekule kwa kauli
moja imemtia hatiani Ngirabatware kwa mashitaka ya mauaji ya kimbari,
uchochezi na ubakaji kama uhalifu dhidi ya binadamu. Katika hukumu
yake,mahakama imemtia hatiani Waziri huyo wa zamani kwa mauaji ya
kimbari kutokana na ukweli kwamba alichochea, kusaidia na kuunga mkono
mashambulizi na mauaji dhidi ya Watutsi katika wilaya yake ya
Nyanyumba, mkoa wa Gisenyi, Kaskazini mwa Rwanda alikozaliwa.
RWANDA
Kesi ya Mugesera yaanza kusikilizwa: Kesi inayomkabili mwanasiasa
mkongwe wa Rwanda, Leon Mugesera ilianza kusikilizwa rasmi Jumatatu
mbele ya Mahakama Kuu mjini Kigali.Hata hivyo mawakili wake wanadai
kuwa kesi hiyo iko nje ya mamlaka ya mahakama hiyo.Kesi imeahirishwa
hadi Desemba 24,mwaka huu. Mugesera anashitakiwa kwa kuchochea mauaji
ya kimbari katika hatuba yake aliyoitoa mwaka 1992.
Jaji wa Ufaransa akataa kuwarejesha Wanyarwanda wawili kwenda kwao:
Jaji mmoja nchini Ufaransa Jumatano alikataa kuwarejesha Kigali
wanyarwanda wawili ikiwa ni pamoja na Waziri wa zamani Hyacinthe
Nsengiyumva Rafiki na afisa mmoja mwandamizi, Venuste Nyombayire. Wote
wawili walishitakiwa kwa kushiriki kwao katika mauaji ya kimbari ya
mwaka 1994 nchini mwao.Mahakama ya mjini Paris, Ufaransa iliamua kwamba
mashitaka ya kutaka kuwarejesha makwao hayana uzito wa kutosha na
inashindikana kuyahusisha moja kwa moja na watuhumiwa hao.
Post a Comment
unashauriwa kutoa maoni muda na wakati wowote na kama unahabari yeyote unaruhusiwa kututumia