Taasisi ya Kimataifa
inayorithi Kazi za Mahakama za Umoja wa Mataifa (MICT),Jumanne
imewaachia huru kabla ya muda wao wa adhabu kuisha, wafungwa wawili huku
Mwendesha Mashitaka wa Mahakama ya Kimataifa ya Makosa ya Jinai (ICC),
Fatou Bensouda alihutubia Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa.
ICTR
Wafungwa wawili waachiwa huru mapema: Taasisi ya Kimataifa inayorithi
Kazi za Mahakama za Umoja wa Mataifa (MICT),Jumanne imewaachia huru
kabla ya muda wao wa adhabu kuisha, wafungwa wawili waliokuwa
wanatumikia kifungo baada ya kutiwa hatiani kwa mauaji ya kimbari ya
Rwanda ya mwaka 1994.Watu hao ni pamoja na meya wa zamani wa wilaya ya
Gikongoro, mkoa wa Kigali Vijijini, Paul Bisengimana na kiongozi wa
zamani wa wanamgambo wa Interahamwe mkoani Gisenyi, Omar Sereshago.
Wawili hao walikuwa wanatumikia adhabu zao nchini Mali.
Wanne waomba hifadhi Ufaransa: Msemaji wa Mahakama ya Kimataifa ya
Mauaji ya Kimbari ya Rwanda (ICTR), Roland Amoussouga ametangaza kwamba
maafisa watatu wa zamani wa serikali ya Rwanda walioachiwa huru na
mahakama hiyo pamoja na afisa mmoja wa jeshi la nchi hiyo, aliyemaliza
kutumikia adhabu yake, wameiomba Ufaransa iwapatie viza ya muda mrefu ya
kuishi nchini humo, ili waweze kuungana na familia zao zinazoishi
katika nchi hiyo.
RWANDA
Meya wa zamani ahukumiwa kifungo cha maisha jela: Jumatano wiki hii,
Mahakama Kuu nchini Rwanda, ilimhukumu meya wa zamani, Jean Pierre
Sewabeza kifungo cha maishan jela baada ya kumtia hatiani kwa kuhusika
kwake katika mauaji ya kimbari ya Rwanda mwaka 1994.
ICC
Mahakama yaiamuru Libya kumkabidhi Abdullah al-Senussi: Jumatatu
majaji wa mahakama ya ICC walitoa amri kwa serikali ya Libya kutekeleza
hati ya kumkamata Abdullah al-Senoussi. Mahakama hiyo inamshitaki Mkuu
huyo wa zamani wa Idara ya Usalama katika utawala wa kiongozi wa zamani
wa Libya, Muammar Gaddafi kwa uhalifu dhidi ya binadamu.
Rufaa ya kupinga ICC kutosikiliza kesi ya Gbagbo yatupwa: Majaji wa
Mahakama ya Rufaa ya ICC, Jumatano kwa kauli moja walitupilia mbali
rufaa iliyopinga mahakama ya ICC kutokuwa na uwezo wa kusikiliza kesi ya
aliyekuwa Rais wa Ivory Coast, Laurent Gbagbo. Hivi sasa Gbagbo
anakabiliwa na kesi ya uhalifu dhidi ya binadamu mbele ya mahakama
hiyo.
Bensouda ahutubia Baraza la Usalama la Umoja wa Mataiafa: Mwendesha
Mashitaka wa ICC, Fatou Bensouda Jumanne alihutubia Baraza la Usalama la
Umoja wa Mataifa mjini New York na kuliomba msaada wa kuwatia mbaroni
watuhumiwa. Alisema tangu mahakama yake itoe hati za kukamtwa kwa
watumiwa kwa mashitaka ya mauaji ya kimbari, uhalifu dhidi ya binadamu
na uhalifu wa kivita dhidi ya maafisa waandamizi wanne, akiwemo mkuu wa
nchi, Omar Al-Bashir, hakuna hata mmoja wao aliyeletwa mbele ya mahakama
hiyo kujibu tuhuma zake.
Kesi ya Bemba yaahirishwa hadi Machi mwakani: Majaji wa mahakama ya
ICC, Alhamisi waliahirisha kusikiliza kesi ya utetezi inayomkabili
Makamu wa Rais wa zamani wa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo (DRC), Jean
Pierre Bemba, anayeshitakiwa kwa uhalifu dhidi ya binadamu na uhalifu
wa kivita.
WIKI IJAYO
ICC
Hukumu ya Ngudjolo kutolewa wiki ijayo: Jumanne ijayo, Desemba 18,
majaji wa ICC watatoa hukumu katika kesi inayomkabili Mathieu Ngodjolo
anayeshitakiwa kwa uhalifu dhidi ya binadamu na uhalifu wa kivita kwa
madai ya kushiriki kwake katika mashambulio ya Bogoro, katika wilaya ya
Ituri, Mashariki mwa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo, Februari 24,
2003.
ICTR
ICTR kutoa hukumu yake ya mwisho: Alhamisi ijayo, majaji wa watotoa
hukumu katika kesi ya mwisho kuwahi kusikilizwa na ICTR inayomhusu
Waziri wa zamani wa Mipango wa Rwanda, Augustin Ngirabatware.
Anashitakiwa kwa kula njama za kufanya mauaji, mauaji ya kimbari au
kushiriki mauaji ya kimbari,uchochezi na uhalifu dhidi ya binadamu.
RWANDA
Kesi ya Mugesera kuanza kuunguruma wiki ijayo: Kesi ya mwanasiasa wa
zamani wa Rwanda, Leon Mugesera inatarajiwa kuanza kusikilizwa Jumatatu
ijayo, Desemba 17,mbele ya Mahakama Kuu ya Rwanda. Mugesera anakabiliwa
na mashitaka ya kuchochea mauaji ya kimbari kupitia hotuba aliyoitoa
katika lugha ya Kinyarwanda mwaka 1992 katika mkutano wa chama chake cha
siasa, Kaskazini mwa Rwanda.
Post a Comment
unashauriwa kutoa maoni muda na wakati wowote na kama unahabari yeyote unaruhusiwa kututumia