Taasisi ya Kimataifa inayorithi Kazi za Mahakama
za Umoja wa Mataifa (MICT),Jumanne imewaachia huru kabla ya muda wao wa
adhabu kuisha, watu wawili waliokuwa wanatumikia kifungo baada ya
kutiwa hatiani kwa mauaji ya kimbari ya Rwanda ya mwaka 1994.
Watu
hao ni pamoja na meya wa zamani wa wilaya ya Gikongoro, mkoa wa Kigali
Vijijini, Paul Bisengimana na kiongozi wa zamani wa wanamgambo wa
Interahamwe mkoani Gisenyi, Omar Sereshago. Wawili hao walikuwa
wanatumikia adhabu zao nchini Mali.
Wakati
anaachiwa,Bisengimana alikuwa ameshatumikia theluthi mbili ya kifungo
cha miaka 15 alichopewa.Alikuwa kizuizini tangu Desemba 4, 2001.
Meya
huyo alitiwa hatiani Aprili 13, 2006 kwa kusaidia na kuunga mkono
kutendeka kwa uhalifu wa kuua na kuteketeza kizazi kama uhalifu dhidi ya
binadamu baada ya yeye mwenyewe kukiri makosa hayo.
Serushago
kwa upande wake ameachiwa akiwa ameshatumikia robo tatu ya kifungo cha
miaka 15 jela alichopewa Februari 5, 1999 baada ya kutiwa hatiani kwa
mauaji ya kimbari na uhalifu dhidi ya binadamu. Kiongozi huyo wa
wanamgambo alikuwa kizuizini tangu Juni 9, 1998. Yeye pia kama alivyo
mfungwa mwenzake alikiri kwa hiari yake mashitaka hayo dhidi yake.
Katika
uamuzi uliomhusu Bisengimana, Rais wa MICT, Jaji Theodor Meron alisema,
‘’Baada ya kuchambua kwa makini vipengele vilivyomo katika sheria na
pia mazingira maalum ya kesi ya Bisengimana, nimeonelea kwamba
anastahili kuachiwa huru mapema na mara moja.’’ Alimwelekeza Msajili
kuifahamisha serikali ya Mali juu ya uamuzi huo.
Uamuzi
wa MICT ambayo ilianzishwa rasmi 2010 kurithi kazi za mahakama mbili za
Umoja wa Mataifa ikiwa ni pamoja na Mahakama ya Kimataifa ya Mauaji ya
Kimbari ya Rwanda (ICTR) na Mahakama ya Kimataifa ya Uhalifu katika
Yogoslavia ya zamani (ICTY) imeonekana kutatua mgogoro wa kisheria wa
muda mrefu kati ya mahakama hizo mbili juu ya suala hilo.
Katika
ICTR, mfungwa anatakiwa kutumikia robo tatu ya adhabu aliyopewa kabla
ya kufikikiriwa kuachiwa huru mapema wakati ICTY, uamuzi kama huo
unaweza kutolewa iwapo mfungwa atakuwa ameshatumikia theluthi mbili ya
adhabu yake.
Lakini
katika uamuzi wake, Rais Meron alisema ‘’Nimeonelea kwamba wafungwa
wote wanaosimamiwa na MICT wanastahili kutendewa sawa.’’
habari hii imeandikwa na mdau wa libeneke la kaskazini Nicodemus Ikonko, Hirondelle, Arusha
Post a Comment
unashauriwa kutoa maoni muda na wakati wowote na kama unahabari yeyote unaruhusiwa kututumia