MWENYEKITI
wa CCM mkoa wa Arusha Onesmo Nangole amesema chama chake kimetangaza rasmi vita
kali dhidi ya watendaji wa serikali wakiwemo wakurugenzi wa halmashauri,wakuu
wa wilaya na wakuu wa mikoa watakaozembea kufanya kazi zao na kwamba
kitawaondoa madarakani.
Nangole
aliyasema hayo jana alipokua akifungua kikao cha baraza la vijana wa CCM (UVCCM)
mkoa wa Arusha kilichofanyika katika hoteli ya Goldenrose jijini Arusha.
Alisema
watendaji hao wa serikali kushindwa kufanya kazi zao kikamilifu ni sawa na
kuwagombanisha wananchi na CCM kwakua kiliingia mkataba nao wa kuwafanyia kazi za
kuwaletea maisha bora kwa miaka mitano mingine.
Alisema
kamwe yeye kama mwenyekiti hawezi kukalia
kimya viongozi hao wazembe kwakua siku ya mwisho watakaoulizwa sio wao bali ni
viongozi wa chama waliohusika katika mkataba huo na wananchi.
Alisema
haiwezekani wao kukubali kuwekwa katika mazingira magumu ya utendaji wao kazi
katika chama kwa uzembe wa viongozi wachache wanaoshindwa kusimamia na
kutekeleza ilani ya chama chake iliyompa ridhaa ya kukalia kiti hicho.
Aliongeza
kuwa katika maeneo mbalimbali viongozi hao wa serikali hasa wakurugenzi wa
halmashauri na majiji wamekuwa wakitengeneza vita na kuwagombanisha viongozi wa
chama na wananchi kutokana na kodi mbalimbali zilizoonekana kuwa kero na
zilizoamuliwa kufutwa.
Akizungumzia
wakuu wa wilaya Nangole alisema baadhi yao
wamekuwa hawaonekani pindi wanapofuatwa na wananchi ofisini kwao ili kuomba
msaada wa kero zao mbalimbali hali inayowakatisha tama wananchi hao na kukosa
imani na serikali yao.
Alisema
hali hiyo imekua ikiendelea kulea vidonda mbalimbali na kuacha makovu kwa
wananchi hao na kubaki na maswali vichwani mwao bila majibu yake wakati wa
kutoa majibu hayo ni wao ila wamekataa kuifanya kazi yao hiyo.
Katika
kikao hicho wajumbe wa watano walichaguliwa kuunda kamati ya utekelezaji ambapo
kwa wilaya ya Arusha alichaguliwa Amina Msangi,KaratuJackob Doday,wilaya ya
Meru Titto Nassari,Arumeru Noel Severe na Monduli Diwani Kimey huku katika
nafasi ya katibu hamasa alichaguliwa kwa mara nyingine mtoto wa mbunge wa
Monduli Edward Lowassa,Fred Lowassa.