Naibu Katibu Mkuu wa chama cha NCCR-Mageuzi (Bara) Lawrence Surumbu Tara na Diwani wa kata ya Bashnet Wilaya ya Babati Mkoani Manyara (katikati) akizungumza na waandishi wa habari jana mjini Babati ambapo alitangaza rasmi kujivua udiwani na vyeo vyote alivyokuwa navyo NCCR-Mageuzi na kujiunga na Chadema (kushoto) ni aliyekuwa mbunge wa Arusha Godbess Lema na,Kamanda Ally Bananga. 


DIWANI WA Kata ya Bashnet Wilayani na Naibu Katibu Mkuu wa NCCR Mageuzi,Lawrence Surumbu Tara amejivua uanachama wa chama hicho na kujiunga na Chadema.

Tara  alitangaza uamuzi huo jana mjini Babati mbele ya waandishi wa habari akiwa na Mjumbe wa Kamati kuu ya Chadema Godbess Lema na kiongozi mwingine wa Chadema Ally Bananga.

Akizungumza wakati akitoa tamko lake la kujitoa NCCR Mageuzi na kujiunga na Chadema,Tara alisema amejitoa kwenye chama hicho akiwa na sababu kuu mbili zilizosababisha yeye kuhama chama hicho.

Alizitaja sababu hizo kuwa ni baadhi ya viongozi wa NCCR Mageuzi kupendelea au kuendeleza urafiki na mfumo dhalimu wa dhuluma na maovu yanayofanywa na dola chini ya Serikali ya CCM.

Alisema kutokana na hali halisi ya kisiasa nchini ilipofika na kwa jinsi dhuluma na maovu kushamiri nchini kiasi cha kufikia watumishi na viongozi wa umma kudhulumu na kufanya maovu kwa uhuru mkubwa bila hofu ya kuadhibiwa.

Alisema wanahitajika chama cha siasa,kilicho makini na ambacho watanzania tunapaswa kuunganisha nguvu zetu kwa pamoja bila kutengana na kwa maoni yangu NCCR Mageuzi siyo chama cha aina hiyo.

Alisema yeye ni mmoja wa waathirika wa mfumo huo mbovu wenye dhuluma kwani alidhulumiwa ubunge kwenye uchaguzi wa mwaka 2010 na kwa bahati mbaya wizi huo wa kura unaongeza maovu.

Alisema katika mazingira hayo amebakiwa na chaguo moja wapo kati ya kubaki ndani ya chama kisichokerwa na wizi wa kura na ambao baadhi ya viongozi wake wanaendeleza urafiki na mfumo huo uliokithiri.

Alisema aliona kujitenga na kuachana na chama chenye viongozi wa aina hiyo na kutafuta chama imara ambacho hakina simile na mambo kama ya aina hio chenye kupigania haki,ukweli na ambacho kimepania utawala bora na ustawi wa watanzania.

Alisema ana amini Chadema ni chama makini kilichopania kutokomeza dhuluma,maovu na ufisadi wa kidola na kuleta ustawi wa Tanzania na aliwaomba wana Bashnet,wana Manyara na watanzania kumuunga mkono.

Naye,Mjumbe wa Kamati kuu ya Chadema,Godbess Lema alimpongeza Tara kwa kujiunga na chama hicho kwani uwezo wake ni mkubwa na hakupaswa kuwa kwenye aina ya chama alichokuwepo awali.

Alisema viongozi wa chama chake badala ya kumpa ushirikiano ili aweze kushinda ubunge baada ya kuibiwa kura za ubunge mwaka 2010,Mwenyekiti wake akakubali kupewa ubunge wa viti maalum na Rais hivyo Tara kuachwa mwenyewe.

Alisema Tara anatarajiwa kupewa kadi ya chama hicho na Mwenyekiti wa Chadema Freeman Mbowe au Katibu Mkuu wa Chama hicho Dk Wilbroad Slaa kwani yeye hawezi kumpa kutokana na nafasi kubwa aliyokuwa nayo.