HOJA tatu za msingi zinatarajiwa kutumiwa na Jopo la Majaji
watatu wa Mahakama ya Rufani, kuamua rufaa ya kesi ya aliyekuwa mbunge
wa Arusha Mjini, Godbless Lema katika hukumu inayotarajiwa kusomwa leo
jijini Dar es Salaam.
Kati ya hoja 18 zilizowasilishwa na upande wa rufaa kupinga hukumu hiyo, zipo hoja tatu ambazo zinaonekana za msingi katika hukumu ya leo itakayotolewa na majaji waliokuwa wakisikiliza kesi hiyo; Salum Massati, Bernard Luanda na kiongozi wao, Nathalia Kimaro.
Lema alivuliwa ubunge Aprili 5, 2012 katika hukumu iliyotolewa na Jaji Gabriel Rwakibalira, kutokana na kesi iliyofunguliwa na makada watatu wa CCM; Mussa Mkanga, Happy Kivuyo na Agnes Mollel, wakipinga ushindi wake katika Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2010.
Kutokana na hukumu hiyo, Lema, kupitia kwa Wakili wake, Method Kimomogoro alikata rufaa Mahakama ya Rufani, akiwasilisha hoja 18 za kupinga hukumu hiyo.
Hoja ya kwanza ni kama mpigakura anaweza kufungua kesi mahakamani kupinga matokeo ya uchaguzi kwa niaba ya mgombea husika aliyeshindwa katika kinyang’anyiro cha uchaguzi.
Wakili Mkuu wa Serikali, Timon Vitalis alidai kuwa Mahakama Kuu Kanda ya Arusha ilikosea kutengua ubunge wa Lema, kutokana na kesi iliyofunguliwa na walalamikaji wanaodai kuwa ni wapigakura.
Wakili Vitalis, aliyemwakilisha Mwanasheria Mkuu wa Serikali (AG), ambaye pia alikuwa upande wa Lema, alidai kuwa wajibu rufaa hawakuwa na haki ya kufungua kesi kupinga ushindi wa mrufani (Lema) kwa kasoro zilizotokea wakati wa kampeni.
Vitalis alidai kuwa, wajibu rufani hao hawakuwa wahusika katika mchakato huo wa kampeni na hivyo hawakuwa na haki ya kupinga matokeo hayo mahakamani.
Akifafanua zaidi, Wakili Vitalis alidai kuwa anayepaswa kufungua kesi mahakamani kwa madai ya lugha ya matusi ni yule aliyetukanwa kwa kuwa hayo ni maumivu ya mtu binafsi na kwamba hata anapokufa, madai yake nayo hufa wala hayawezi kuendelezwa na mtu mwingine.
“Sasa iweje kwa mtu ambaye yuko hai, lakini watu wengine ndio waje mahakamani kufungua kesi? Alihoji Wakili Vitalis.
Hoja hiyo iliungwa mkono na mawakili wa mrufani, Method Kimomogoro na mwenzake ambaye pia ni Mbunge wa Singida Mashariki (Chadema), Tundu Lissu.
Wakili Kimomogoro alidai kuwa, Jaji alikosea kuamua kuwa mtu yeyote aliyejiandikisha kupiga kura ana haki isiyo na mpaka ya kufungua kesi kupinga matokeo.
Alidai kuwa, hoja yao ni kwamba mtu anakuwa na haki hiyo pale ambapo haki yake imevunjwa au inaelekea kuvunjwa na si pale aliyeathirika na ukiukwaji wa haki hiyo ni mtu mwingine.
Kwa upande wake, Lissu alidai kuwa mpigakura ana haki ya kupinga matokeo mahakamani kwa madai kuwa haki zake pale ambapo madai yao yanaambatana na haki zilizotajwa kwenye Katiba ambazo ni pamoja na haki ya kupiga kura.
Majibu ya Warufaniwa
Akijibu hoja hiyo, Wakili wa warufaniwa, Alute Mughway alidai kuwa haki hiyo inaelezwa katika kifungu cha 111 (1) (A) cha Sheria ya Uchaguzi (2010) pamoja na Katiba na sheria nyingine za nchi na Kanuni za Maadili ya Uchaguzi zinazokataza siasa za majitaka.
Uamuzi wa Mahakama kuhusu hoja hiyo ndiyo ama utahitimisha hukumu hiyo bila kujadili na kuzitolea uamuzi hoja nyingine, ikiwa mahakama itaamua kuanza na hoja hiyo, au utakaoruhusu kuendelea na mjadala na kisha uamuzi wa hoja nyingine kutolewa.
Chanzo mwananchi