MKE wa askari polisi wa kikosi cha usalama barabarani
(trafiki), Sajenti Ally Salum (Kinyogori) aliyeuawa hivi
karibuni, inadaiwa amekiri kuhusika kwenye mauaji hayo,
akidai ilitokana na mumewe kumuacha na kuoa mke
mwingine.
Kamanda wa Polisi, Kanda Maalumu ya Dar es Salaam, Simon
Sirro aliwaambia waandishi wa habari jana kuwa mwanamke
huyo anashikiliwa na polisi kwa mauaji hayo yaliyofanyika
nyumbani kwa Kinyogori, Mkuranga mkoani Pwani.
Wakati huo huo, Kamanda Sirro amezungumzia pia mauaji ya
Anathe Msuya yaliyofanyika hivi karibuni Kigamboni na
kusema polisi inaendelea kumtafuta msichana wa kazi za
nyumbani aliyetoroka siku moja kabla ya kifo cha
mwanamke huyo.
Anayetuhumiwa kuua mumewe
Akizungumza na waandishi wa habari jana kuhusu matukio
mbalimbali ya uhalifu yaliyojitokeza jijini Dar es
Salaam, Sirro alisema katika mahojiano ya awali mke wa
Kinyogori amekiri kuhusika.
Kwa mujibu wa kamanda, mwanamke huyo ambaye hata hivyo
hakutaja jina lake kwa sababu za kipelelezi, aliamua
kumtuma mtu kutekeleza mauaji hayo baada ya mumewe
kumwacha na kuoa mke mwingine.
“Ni jambo la kusikitisha kuona mtu anatoa uhai wa mtu
sababu ya kuachwa. Tunawasihi wananchi kuepuka
kujihusisha na matukio kama haya, eti sababu tu ya
kuachwa wanawake wapo wengi na wanaume wapo wengi
unaweza kuachwa na ukaolewa na ukaoa kuliko kuondoa uhai
wa mtu,” alisisitiza Sirro.
Hata hivyo, Sirro alisema wanaendelea kuwahoji
watuhumiwa hao ili waweze kuwataja watu wengine
walioshirikiana nao kutekeleza tukio hilo baada ya
kuonekana kuwepo kwa wahusika wengine.
‘Hausigeli’ asakwa
Kuhusu mauaji ya Anathe aliyechinjwa nyumbani kwake
Kibada, Kigamboni, Kamanda Sirro alisema wanaendelea na
jitihada za kumtafuta msichana huyo ahojiwe kuhusu tukio
hilo.
Aidha alisema mtu mmoja anashikiliwa akituhumiwa
kuhusika na tukio hilo huku polisi ikiwa imeandaa timu
ya upelelezi itakayoshughulikia tukio hilo kufanikisha
kuwakamata wote waliohusika na tukio hilo.
Sirro alisema msichana huyo aliondoka siku moja kabla ya
tukio hilo la mauaji hivyo kupatikana kwake, kunaweza
kusaidia polisi kujua kama kuondoka kwake kulikuwa salama
au kuna kitu kimejificha.
“Msichana huyu tunaendelea kumsaka tujue kama aliondoka
salama na kumhoji zaidi juu ya kuondoka kwake siku moja
tu, tukio linatokea nina imani tutafanikiwa kumpata na
wote waliohusika na kukomesha matukio haya,” alisema
Sirro.
Mamia wajitokeza msibani
Vilio na simanzi jana vilitawala wakati mamia ya wakazi
wa Kibada Kigamboni na Salasala walipokuwa wakiuaga mwili
wa marehemu Anathe Msuya (30), aliyeuawa Mei 25 nyumbani
kwake kwa kuchinjwa na watu wasiojulikana.
Mwili ulichukuliwa jana asubuhi kutoka Hospitali ya
Taifa Muhimbili na kupelekwa nyumbani kwake Kibada, kwa
ajili ya kuagwa na majirani zake kabla ya kusafirishwa
kwenda kuzikwa mkoani Arusha leo.
Akizungumza baada ya mamia kumuaga nyumbani kwa
marehemu, mwenyekiti wa serikali ya mtaa wa Nyakwale
Kibada, Said Pazi alisema kuwa wao kama majirani
waliomba familia wapate fursa ya kumuaga jirani yao
ambaye tangu ahamie ana muda wa miezi sita.
“Baada ya kuambiwa msiba upo Salasala tuliomba kama
majirani na sisi tupatiwe fursa ya kuuaga mwili wa ndugu
yetu ambaye alihamia mwaka jana… kwa kweli msiba wake
umetusikitisha sana” alisema.
Akizungumzia tukio hilo alisema kuwa mtoto wa marehemu
huyo, Allan Kimario (4) aliwataarifu majirani kuwa mama
yake haamki na ndipo walipofika wakakuta ameuawa.
Mwenyekiti huyo alitoa pole na kusema atahakikisha
wanaimarisha ulinzi na kuhimiza wenye viwanja ambavyo
havijajengwa, wavifanyie usafi ili kuondoa vichaka ambavyo ni hatari kwa usalama.