Meya wa Jiji la Dar es Salaam, Charles Mwita
Meya wa Jiji la Dar es Salaam, aliyetokana na
vyama vinavyounda Umoja wa Katiba ya Wananchi (Ukawa), Charles Mwita,
amesema mikatata tata iliyoingiwa na Jiji ukiwamo ule wa mabasi yaendayo
kasi (Dart) na Shirika la Usafiri Dar es Salaam (Uda) pamoja na ule wa
Kituo cha Mabasi Ubungo, itapitiwa upya na wanasheria kisha taarifa zake
kuwekwa wazi kwa umma.
Akizungumza na Nipashe katika mahojiano maalum mwishoni mwa wiki,
Meya Mwita alisema: “Tutaita wanasheria na tutaipitia hadharani na
tutawaeleza wananchi. Nina siku tatu ofisini, nipeni muda zaidi
nitaeleza tuliyobaini kwenye mikataba husika.”
Meya huyo ambaye alichaguliwa na madiwani wa Chadema na wa CUF,
alisema hakutakuwa na ubabaishaji katika mikataba hiyo kwani ndiko
mapato mengi yanakopotea na kusababisha miradi ya maendeleo inayohudumia
wananchi wengi kukwama ama kutotelekezwa.
“Ninachotaka bora mimi nife, lakini wananchi mpate haki, mmekuwa
maskini kwa muda mrefu sana, mmedharauliwa vya kutosha, haiwezekani nchi
ni yetu sote, siyo ‘majitu’ fulani yanakuja hapa yanatengeneza genge la
wizi na kutajirika, wakati raslimali zipo na fedha za kutekeleza miradi
ipo, kinachotakiwa ni usimamiaji na ufuatiliaji kuhakikisha hakuna
shilingi inapotea,” alisisitiza na kuongeza.
“Tutaheshimiana hapa mjini Mungu ndiye ametupa Dar es Salaam,
tutawatumikia sana kwa nguvu zote,” alisema Mwita ambaye ni diwani wa
kata ya Vijibweni.
Meya huyo alianza na mradi wa Uda kuwa atahitaji ripoti kutoka kwa
waliokuwepo na kusoma kwa undani ndipo atakuwa katika nafasi nzuri ya
kulizungumzia.
"Kituo cha Ubungo, mwaka jana kulikuwa na mpango wa kukihamisha
kwenda Mbezi, lakini hadi sasa hakuna kilichofanyika, ninachosubiri ni
ripoti ya kwanini waliamua kubomoa kabla hawajamaliza kujenga kituo
mbadala," alisema na kuongeza.
“Tutaamua kwa pamoja katika kikao chetu cha Jiji kwamba tutaendelea
na kituo kilichopo au Mbezi. Nina jambo la dharura nitakwenda kulifanya
juu ya kituo hiki ambacho kinatoza fedha kwa watumiaji, lakini hakuna
huduma za choo, kujikinga na jua na mpangiliop kwa ujumla,” alisema.
BODABODA
Meya huyo alisema hatakubaliana na kamatakamata ya waendesha
pikipiki inayofanyika maeneo mbalimbali ya Jiji kwa kuwa vijana
wanajitafutia riziki ya kuendesha familia zao.
“Hawa ni Watanzania wenzetu ambao serikali iliwanyima elimu, mtu
akijiajiri tumuonee huruma, tumsaidie na siyo kumfanya awe maskini
zaidi,” alisema.
Meya Mwita alisema suala la pikipiki kuingia katikati ya Jiji
litajadiliwa kwenye vikao na kusikiliza walioamua kuwazua kwanini
walifanya hivyo na kama inawezekana kuweka utaratibu wa muda wa kuingia
na kutoka.
Alisema wengi wanakamatwa kwa makosa ya leseni, lakini
kinachoonekana ni kukosekana kwa elimu, hivyo Polisi na Mamlaka ya
Mapato nchini (TRA) kuwaelimisha umuhimu wa kuwa na leseni na bima za
vyombo vyao.
“Nitaendelea kutoa elimu kwenye vyombo vya habari, nitawakusanya
waendesha bodaboda wote nitaongea nao, pia madiwani wa vyama vyote
tujadili kwa kina na kuwa na utaratibu maalum kwa ajili yao nao watoe
elimu ya uraia kwenye kata zao,” alisema.
SOURCE:
NIPASHE