ASKARI WAWANYAPORI WADAI KUWATESA WAFUGAJI,KWA KUWADUMBUKIZA KWENYE MAJI

 Picha mbalimbali za wafugaji wa kijiji cha Handa,katika wilaya ya Chemba,wakiwa kwenye mkutano wa hadhara wakilalamikia hatua ya askari wa wanyama pori kuwatesa ikiwemo kuwadumbukiza kwenye kina kirefu cha maji pindi mifugo yao inapoingia kimakosa kwenye eneo Tengefupicha na Joseph Ngilisho wa libeneke la kaskazini blog 



Askari wa wanyama pori katika Pori Tengefu la Swaga Swaga lililopo kijiji cha Handa ,Kwa Mtoro wilaya ya Chemba ,mkoa wa Dodoma,wanadaiwa kuwatesa  wafugaji wa kijiji hicho pindi  mifugo yao imeingia kimakosa katika pori hilo kwa kuwachapa mijeredi na kuwaning’iniza kwenye kina kirefu cha maji.

Aidha wanadaiwa kuwatozwa faini kubwa wafugaji hao bila kuwapa stakabadhi ya malipo pindi wanapokamata mifugo yao inapokuwa imeingia kwenye pori hilo,kinyume cha sheria

Wakizungumza kwenye mkutano wa hadhara uliofanyika  kijiji hapo, wamedai kuwa vitendo hivyo ni ukiuka wa haki za binadamu ,kwani haadhi yao wamepata majeraha ya kudumu kwa sababu ya kipigo.

Samweli Hondi ,akizungumza kwa niaba ya wenzake huku akionyesha majeraha kadhaa  yaliyotokana na  kipigo alisema,askari hao hulazimika kuifuata mifuga yao hata kwenye maboma yao na kuiswaga hadi kwenye kambi yao na kumtaka mmiliki wa mifugo hiyo afike kambini kuikomboa.

‘’Unajua hawa askari wamewafanya wafukaji kama mashine ya kutolea hela ATM,wanapokuwa hawana hela hulazimika kuja kwenye maboma ya wafugaji na kuswaga mifugo yote ,huku wakimwambia mfugaji aje kambini kukaomboa’’alisema Hondi

Naye mwenyekiti wa kijiji hicho,Sunta Ramadhani alieleza kuwa kijiji cha Handa kimesajiliwa kihalali kama makazi halali ya  wananchi,lakini alikiri kuwepo kwa mgogoro baina ya wanakijiji na eneo hilo na hifadhi ya wanyama pori.

Alisema askari hao wamekuwa wakiwakamata wafugaji na kuwalazimisha kulipia mifugo yao,malipo ambayo hayana kiwango maalumu na hukadilia kutokana na mwonekano wa mfugaji.

Aliongeza kuwa askari hao waliwahi kuwataka wafugaji hao wawapatie kiasi cha shilingi milioni 3 ili wawaruhusu waendelee kunywesha mifugo yao kwenye visima vya maji vilivyoko ndani ya hifadhi hiyo,lakini baada ya kukabidhiwa kitita hicho,waliwaruhusu kunywesha mifugo kwa siku moja na baadae waliendelea kuwazuia.

‘’Tulichangishana shilingi elfu 25 kila kaya na kufanikiwa kupata kiasi hicho cha fedha tulichowakabidhi chaajabu waliruhusiwa kunyesha mifugo yetu siku moja tu na kutuzuia’’alisema Mwenyekiti huyo na kuongeza.

''Leo hii tunapoongea mwenzetu mfugaji amekamatiwa jana ng'ombe wake na amelipa faini ya shilingi 800,000 na hakupewa lisiti yoyote tutaishi hivi mpaka lini''

Naye mfugaji ,Justine Matata alisema wanakijiji zaidi ya 20 waliwahi kukamatwa na kuteswa na kisha kutozwa faini zisizo na stakabadhi ya malipo,huku akidai kuwa askari hao wamewageuza mashine ya kutolea fedha ATM.

Alisema mnamo februali 2,mwaka huu ng’ombe wake 43 alikamatwa na kutozwa faini ya shilingi 800,000 hata hivyo aliomba apewe lisiti ya malipo lakini alijikuta akiambulia kipigo kutoka kwa askari hao.

Wafugaji zaidi ya 20 mkutanoni hapo walijitokeza na kukiri kudhalilishwa na askari hao ikiwemo kutozwa faini bila kupewa stakabadhi ya malipo baada ya kukamatiwa mifugo yao.

Baadhi ya wafugaji hao ni pamoja na Samweli Hondi aliyetozwa sh,220,000,oktoba 18,2014 na Juma Hondi sh,260,000 oktoba 18,2014.

Wengine ni Kambona Cremence sh,300,000 oktoba 18 mwaka 2014,Athumani Msabaha sh,200,000 oktoba 19 mwaka 2014 ,Said Abrahaman sh.400,000 oktoba 11 mwaka 2014 na Omary Mukya sh 300,000 oktoba 11 mwaka 2014.

Wengine ni Adam Jumanne sh,600,000 ambaye alikamatiwa ng’ombe  70,Silanjini Soya sh,400,000,James Margwe sh,500,000 Juma Seleman 400,000 na Jerad Mgoo sh,250,000.

Gazeti hili lilifanikiwa kufika kwenye kambi ya askari hao ,ambapo pamoja na kudai si wasemeji wa idara ya wanyama Pori,walikana kuhusika na madai hayo na kudai kuwa wananchi wanawachafua.

‘’Si kweli kama tunawapiga na kuwadhalilisha hayo sasa ni kuchafuana nahisi haya masuala yameingia siasa ,sisi tupo hapa kwa mujibu wa sheria na hatumwonei mtu’’alisema mmoja wa askari hao ambaye hakutaka kutaja jina lake.

Aliongeza kwa kudai kuwa mipaka ya hifadhi inajulikana na kwamba hatua ya wafugaji kudai hawaijui si kweli kwani kulikuwepo na mabango yanayoelekeza lakini kila yakiwekwa wanayang’oa.

Kwa upande wa waziri wa utalii na mali asili ,Lazaro Nyalandu akizungumza ka njia ya simu alisema kuwa taarifa hiyo ndo ameipata na aliahidi kuifanyia kazi .

Aliongeza kuwa wizara yake imeandaa kikosi maalumu cha kufanya uchunguzi kwenye maeneo yote tengefu ili kubaini kero mbalimbali zilizoko katika maeneo hayo.
Hata hivyo aliahidi kuchukua hatua kali iwapo itathibitika askari hao kujihusisha na vitendo vinavyoenda kinyume na taratibu zai nchi.

‘’kama kweli askari wetu wanafanya hivyo na wanawatoza fedha wafugaji bila kuwapa stakabadhi tutachukua hatua mara moja ila naomba unitumie hayo malalamiko kupitia barua pepe yangu naahidi kuchukua hatua mara moja’’alisema Waziri Nyalandu.






Post a Comment

unashauriwa kutoa maoni muda na wakati wowote na kama unahabari yeyote unaruhusiwa kututumia

Previous Post Next Post