Baadhi ya barabara za manispaa ya Moshi zitafungwa ili kuhakikisha usalama
wa wanariadha wataoshiriki mbio za kimataifa za Kilimanjaro Marathon 2015
zitakazofanyika Jumapili Machi mosi.
Mkurugenzi wa Wild Frontiers, waandaaji wa mbio hizo amesema katika
taarifa yake kwa vyombo vya habari kwamba Halmashauri ya Manispaa ya Moshi
imetoa kibali cha kufunga na takribani kilometa kumi za barabara kuu
iendayo Dar zitafungwa kuanzia saa 12.15 asubuhi hadi saa 2.00 asubuhi.
Barabara ya Sokoine kutokea chuo kikuu cha ushirika na biashara, (MOCU),
hadi KCMC na kona barabara ya Kibosho na kutoka barabara ya Lema hadi chuo
kikuu cha ushirika, kupitia barabara ya Kilimanjaro, zitafunguwa kuanzia
saa 12.30 asubuhi hadi saa 2.00 asubuhi.
Addison alisema kutakuwa na udhibiti utakaofanywa na askari wa usalama
barabarani kwenye barabara ya kutoka YMCA hadi mnara wa Saa, Barabara ya
Boma, mzunguko wa barabara ya Arusha, Barabara ya Uru hadi ile ya chuo
kikuu cha ushirika, zitafungwa kuanzia saa 1.30 asubuhi hadi za 2.15
asubuhi.
"Madereva wote watakaotumia barabara hizi punde zitakapofunguliwa
wanaombwa kuendesha magari yao kwa uangalifu na tahadhari kubwa kwa ajili
ya usalama wa wale wanariadha ambao bado watakuwa wanaendelea na mbio
hizo", alisema.
Makampuni ya kusafirisha na kuongoza watalii watakaokuwana makujukumu ya
kuwasafirisha wateja wao kutokea Mweka, yanashauriwa kuanza safari zao
baada ya Saa 3.00 asubuhi kwa kupitia barabara za Mweka na Sokoine kwa vile
wanariadha watakuwa washapita maeneo hayo.
Waendesha magari na wale wa vyombo vingine vya moto wanashauriwa kuepuka
kutumia barabara za Lema, Kilimanjaro na ile ya lango kuu la kuingilia chuo
kikuu cha ushirika na biashara kadiri itakavyowezekana ili kuepuka usumbufu.
Mabasi ya mikoani yanashauriwa kuanza safari zao za kutoka Moshi kuelekea
Dar es Salaam baada ya Saa 2.00 asubuhi. Hata hivyo yale ya kutoka Moshi
kuelekea Arusha yanaweza kufanya hivyo kwa kupitia barabara ile ya mzunguko
wa barabara ya kwenda Arusha.