Mwenyekiti wa Chama cha Wananchi (CUF),
Profesa Ibrahim Lipumba amesema anatarajia kwenda Ikulu kumwona Rais
Jakaya Kikwete ili kumweleza mambo mbalimbali ikiwamo ubabe na upendeleo
unaofanywa na polisi.
Akizungumza na waandishi wa habari jana, Profesa
Lipumba alisema Chama Cha Mapinduzi (CCM) kimekuwa kikifanya mikutano
bila ya kubughudhiwa na polisi tofauti na inavyofanyiwa CUF.
“Kinana anafanya mikutano kila siku lakini
hatujawahi kuona akibughudhiwa na polisi lakini chama chetu kimekuwa
kikiambulia mabomu ya machozi, vipigo na kuzuia mikutano yetu, Rais
inabidi aingilie kati hasa katika kipindi hiki tunachoelekea katika
uchaguzi mkuu,” alisema.
Profesa Lipumba alisema huko ni kuleta mgawanyiko unaoweza kusababisha machafuko kama hatua madhubuti hazitachukuliwa.
Jumanne iliyopita, Jeshi la Polisi lilizuia
maandamano na mkutano wa chama hicho uliokuwa ufanyike kuadhimisha miaka
14 ya mauaji ya wenzao yaliyotokea Zanzibar Februari 26 na 27, 2001.
Katika tukio hilo, Profesa Lipumba na wafuasi 32
walikamatwa na baadaye kufunguliwa mashtaka mahakamani ya kula njama,
kufanya maandamano na kukusanyika bila kibali. Vitendo hivyo vya polisi
vilisababisha Bunge la Jamhuri ya Muungano kusitisha shughuli zake na
kujadili tukio hilo bila kujali kwamba lilikuwa linaingilia mhimili
mwingine wa nchi.
Jana, Profesa Lipumba alisema: “Nataka kuonana na
Rais Kikwete ana kwa ana, siwezi kumwandikia barua kwa sababu nafahamu
hana muda wa kusoma, hivi sasa nafanya kila juhudi ili kumwona.”
Profesa Lipumba alisema Januari 22, mwaka huu
chama chake kilipeleka barua ya kufanya maandamano na mkutano kwenye
Uwanja wa Zakhem, Mbagala wilayani Temeke na kiliwatangazia wananchi
kwamba maandamano na mkutano huo vingefanyia Januari 27 kuanzia saa 8.00
mchana na maandamano yangeanzia Temeke Mwisho hadi katika uwanja huo.
Alisema Januari 26, saa 12.00 jioni ikiwa imebaki
siku moja, ndipo Jeshi la Polisi likatoa amri ya kupinga kufanyika kwa
maandamano hayo na mkutano.
“Tulishawatangazia wananchi kuhusu maandamano hayo
na mkutano, usiku huo tungewajulisha vipi kufuta mkutano huo, kwa nini
hawakutujulisha mapema? Matatizo kama hayo yanasababishwa na Jeshi la
Polisi,” alisema Profesa Lipumba.
Alisema wakati wakisaini makubaliano ya Serikali
ya Umoja wa Kitaifa kati ya CCM na CUF Zanzibar, alipopewa nafasi ya
kuzungumza alisema: “Tusameheane kwa mauaji yaliyotokea Zanzibar lakini
tusiyasahau kwa sababu tukifanya hivyo yanaweza kujirudia.”
Alisema ndiyo maana kila mwaka, wamekuwa wakifanya kumbukumbu za mauaji hayo ili yasirudie tena
chanzo .mwananchi
chanzo .mwananchi
Post a Comment
unashauriwa kutoa maoni muda na wakati wowote na kama unahabari yeyote unaruhusiwa kututumia