BENDI mpya inayotamba kwa sasa hapa nchini na ambayo
imechukua tuzo mbalimbali za muziki hapa nchini Mashujaa Band Jumapili tarehe 1
Machi inatarajia kushuka mjini Moshi katika ukumbi wa Uwanja wa Chuo cha
Ushirika kuwapa burudani washiriki pamoja na wananchi wote watakaofika kwenye
uwanja huo kwa ajili ya mbio za Kilimanjaro Marathon 2015.
Meneja wa bia ya Kilimanjaro Premium Lager, Pamela Kikuli alisema
kuwa bia ya Kilimanjaro Premium Lager imeandaa burudani hiyo ikiwa ni mojawapo
ya burudani zilizoandaliwa kwa ajili ya kuongeza msisimko katika mbio hizo.
Alisema kuwa siku ya Kilimanjaro Marathon bendi ya Mashujaa
watatoa burudani hiyo kwa kushirikiana na kundi la Jambo Squad kutoka Arusha.
Kikuli aliongeza kuwa Jambo Squad pamoja na Warriors From
The East la Arusha kwa pamoja wataanza kuchangamsha mji wa Moshi kuanzia usiku wa
Ijumaa tarehe 27 ambapo watatoa burudani kabambe kwa wakazi wa Moshi kwenye
ukumbi wa Voda House ikiwa ni burudani mahususi kuelekea Kilimanjaro Marathon.
Mbali na burudani ya muziki siku ya Kilimanjaro Marathon
kutakuwa na burudani mbalimbali katika viwanja hivyo pamoja na nyama choma
kutoka bar mbalimbali maarufu za Moshi ambao watachoma nyama na kuuza vinywaji
uwanjani hapo.
John Addison, Mkurugenzi Mkuu wa Wild Frontiers, waandaaji
wa mbio hizo alisema kuwa wanariadha wanaotaka kushiriki mbio hizo wataweza
kujiandikisha tarehe 26 jijini Arusha kwenye Hoteli ya Kibo Palace na kwa Moshi
watajiandikisha Keys Hotel tarehe 27 na tarehe 28 Februari 2015 kuanzia saa nne
asubuhi mpaka saa 12 jioni.
Aliongeza kuwa mbio ndefu la Kilimanjaro Premium Lager
Marathon za kilomita 42 zitaanza saa 12.30 asubuhi kutokea uwanja wa Ushirika
wakati mbio za Tigo Kili Half Marathon zitaanzia nje ya geti la Chuo cha
Ushirika saa moja kamili asubuhi na kukimbia wakielekea Mweka na mbio yao
itaishia hapo hapo uwanjani. Wakati huo huo mbio za walemavu za Gapco zitaanza
saa 12.45 (saa moja kasorobo) kutokea uwanja wa Ushirika na huku mbio za
kujifurahisha za 5 km Fun Run zikianza saa 1.45 asubuhi kwenye mzunguko wa YMCA
na kumalizikia uwanjani.
Addison alisema kuwa maandalizi ya kutosha yamefanyika
kuhakikisha washiriki wanafurahia mbio hizo kwani kila mdhamini atakuwa na
vituo maalum vya maji ya kunywa na viburudisho na burudani nyingine katika
vituo hivyo ambavyo vitakuwepo kila baada ya kilometa chache katika njia
zitakapopita njia hizo”.
Mbio za Kilimanjaro Marathon 2015 zinaratibiwa na Executive
Solutions kwa kushirikiana na Riadha Tanzania, Riadha Kilimanjaro na
Kilimanjaro Marathon Club huku zikidhaminiwa na Kilimanjaro Premium Lager,
Tigo, GAPCO, Simba Cement, KK Security, Keys Hotel, TPC Sugar, CMC Automobiles Ltd, RwandAir, FNB Tanzania,
Kibo Palace Hotel, UNFPA na Kilimanjaro Water.