Jeshi la Polisi nchini, limesema majambazi waliokuwa wamejificha
katika mapango ya Amboni nje kidogo ya jiji la Tanga wamekimbia.
Mkurugenzi wa Operesheni na Mafunzo wa jeshi hilo, Kamishna Paul
Chagonja, akizungumza jana katika mahojiano na Radio One katika kipindi
cha Kumepambazuka, alisema majambazi hao wamekimbia baada ya kuzidiwa
nguvu na askari wa jeshi lake wanaoshirikiana na Jeshi la Ulinzi wa
Wananchi wa Tanzania (JWTZ).
Hata hivyo, alisema vyombo vya ulinzi na usalama bado vinaendelea
na msako mkali wa kuwabaini na kwamba, watu hao siyo magaidi kama
inavyoelezwa, bali ni majambazi wa kawaida.
“Tunaowasaka siyo magaidi. Wananchi wasiyumbishwe na taarifa ambazo
hazina vyanzo rasmi kutoka serikalini. Wanaodai hao watu ni magaidi
wana sababu zao binafsi,” alisema Kamishna Chagonja.
Alisema Jeshi la Polisi halijapata ushahidi wa kutosha wa
kujiridhisha kuwa watu hao ni magaidi na kwamba walitoroka kupitia
mlango wa pili wa mapango hayo walimokuwa wamejificha.
“Wakati wa kupambana tuliwazidi nguvu, wakatoroka kupitia mlango wa
nyuma upande wa pili na kukimbia kutokana na mapango walimokuwa
wamejificha kuwa na sehemu ya kutokea,” alisema.
Alisema askari walipoingia ndani ya mapango hayo baada ya majambazi
hao kutoroka, walikuta pikipiki, baiskeli na nguo mbalimbali, ambazo
inawezekana walizipora.
Kamishna Chagonja alisema baadhi ya watu wamekuwa wakihoji kuwa
kama watu hao ni majambazi wa kawaida kwa nini washirikiane na JWTZ na
kueleza kuwa ni jambo la kawaida kushirikiana na jeshi kutokana na
mazingira ya tukio, ambalo lilihitaji utalaamu wa kupambana na wahalifu
hao.
“Kushirikiana na JWTZ ni jambo la kawaida kwa sababu mazingira
waliyokuwa wamejificha majambazi hao kulihitajika utaalamu wa namna ya
kupambana nao. Wenzetu wanajeshi wana utalaaamu,” alisema.
Alisema upelelezi unaendelea kubaini majambazi hao waliingiaje
katika mapango hayo na kama walihusika katika uporaji wa silaha katika
maeneo mbalimbali.
Alitoa wito kwa wananchi wakiwaona watu waliojeruhiwa watoe taarifa kwa jeshi hilo.
RC AUNGANA NA CHAGONJA
Mkuu wa Mkoa wa Tanga, Said Magalula, akizungumza na waandishi wa
habari mkoani humo jana, alikanusha kwamba watu kuwa ni magaidi, badala
yake akasema ni majambazi waliohusika na tukio la uporaji wa silaha
mbili aina ya SMG zenye risasi 60 mmkoani humo.
Alisema majambazi hao waliwapora askari polisi silaha hizo
walipokuwa kwenye kibanda cha kinachotumika kuuza chipsi hivi karibuni,
jijini Tanga.
Hata hivyo, alisema mpaka sasa hakuna mtu yeyote aliyekamatwa
kuhusiana na tukio hilo na kwamba hali ni shwari, hivyo, akawataka
wananchi kuendelea na shughuli zao za kiuchumi kama kawaida.
ASKARI ALIYEUAWA AZIKWA
Wakati viongozi hao wakisema hayo, mwili wa askari aliyekufa wakati
wa shambulio hilo, ulizikwa jana katika eneo la Kwashemshi, wilayani
Korogwe, mkoani humo na kwamba, wengine waliojeruhiwa na kulazwa katika
Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Tanga ya Bombo hali zao zinaendelea
vizuri.
WANANCHI WANENA
Wakazi wa Kijiji cha Majimoto, Kata ya Mzizima, jijini Tanga
wameelezea namna walivyoishi na majambazi hao kwa zaidi ya miezi sita
katika kijiji hicho, huku wakiwadhani kuwa ni vibarua wa mashambani.
Majambazi hao wanaodaiwa kusababisha mashambulizi baina yao na
askari polisi na wa JWTZ na kusababisha majeruhi watano na kifo cha
askari mmoja, waliishi kama raia wema kwa kipindi chote hicho katika
kijiji hicho.
Baadhi ya wakazi wa kijiji hicho waliozungumza na NIPASHE walieleza
jinsi majambazi hao walivyokuwa na uchangamfu na ucheshi kila
wanapokutana nao.
Yahya Adam, ambaye ni mkazi wa kijiji hicho alisema, katika kipindi
chote hicho, watu hao walikuwa wakipendelea mashati ya mikono mirefu,
suruali za jeans zilizokatwa chini na kanzu.
“Hawa bwana walikuwa wanavaa short jeans, yaani wamekaa ki-jihad
zaidi na yeboyebo chini. Lakini mashati yao ni ya mikono mirefu na
kanzu. Wakati mwingine walikuwa wanavaa na kofia juu ya balaghashia. Ni
wachangamfu sana. Ukikutana nao huwezi kuwashtukia kama ni wageni, kwani
utahisi wanakujua tu kutokana na salamu za kuchangamka,” alisema Adam.
Bakari Ali alisema watu hao walikuwa wakionekana kwenye maeneo ya
magenge kunapouzwa bidhaa kama unga, dagaa na nyanya wakinunua nyakati
za mchana na kutoweka kusikojulikana.
“Walikuwa wakitembea wawili wawili na walikuwa wakija gengeni
wananunua nyanya, dagaa na hata unga halafu wanashika njia ya porini na
kutokomea. Kusema kweli wote wananchi wa hapa tulikuwa tukijua ni
wakulima,” alisema Ali.
Walisema watu hao walikuwa wakiwaona kila siku majira ya saa 12.00 asubuhi wakitokea eneo la mashambani.
“Kusema kweli mimi ni mpasua mawe, ndiyo shughuli yangu kubwa ya
kiuchumi. Sasa kila siku alfajiri tunapotoka na wenzangu kwenda kazini,
tunakutana na hawa watu. Tukawa tunajua kuwa ni wakulima, kwani kwenye
pori la Mbogo ambako kuna shamba kubwa ndiko tulikuwa tunakutana nao. Na
wanatembea wawili wawili. Leo unakutana na wengine na kesho unakutana
na wengine,” alisema Ali.
Baadhi ya vijana wa kijiji hicho, ambao kazi yao kubwa ni kupasua
mawe, walisema siku ya tukio walikuwa wamekaa kwenye kijiwe chao cha
kila siku, lakini wakashangazwa majira ya saa 5.00 asubuhi kuona gari
mbili za FFU zikipita kuelekea kwenye eneo la machimbo na kuwafanya
wakimbilie huko wakijua kumepatikana madini.
Walisema wakati wakikimbilia eneo hilo wakiwa nane, askari mmoja
aliwafuata na kuwataka wawaelekeze njia kwenye eneo la mapori
walikokimbilia majambazi hao.
Said alisema kilichowatisha ni baada ya kuona wameachwa peke yao porini bila silaha yoyote ya kujihami.
Alisema walipotaka kuondoka, askari hao waliwataka waongozane nao
hadi kwenye mapango ambayo wahalifu hao walikuwa wakiishi, ambako
kulipatikana pikipiki mbili, unga, dagaa, sufuria na baiskeli tatu.
“Pale walipiga mabomu kwanza. Tuliambiwa tuache midomo wazi ili
tusipate madhara. Baada ya mabomu hayo, ndiyo wakaingia kwenye pango na
kukatolewa vitu hivyo. Kusema kweli sisi tulikuwa tumechoka sana.
Tulikuwa na wasiwasi na familia zetu, kwani hakuna aliyekuwa anajua
tumepotelea wapi…na hali mirindimo ya risasi na mabomu ikiendelea,”
alisema.
Alisema kutokana na hali hiyo, yeye na wenzake watano walilazimika
kuwakimbia askari hao na kurudi makwao ili kuondoa hofu kwa familia,
ambazo zilijua tayari nao wamekwishauawa.
Taarifa ambazo hazijathibitishwa ni kwamba vijana hao ni miongoni
mwa waliofuzu mafunzo ya JKT, ambao walifukuzwa na wengine kukosa ajira
na hivyo kuwafanya wakate tamaa ya maisha.
Taarifa hizo zinatokana na mtu mmoja kukamatwa na wakazi wa maeneo
hayo akifua mtoni akiwa na kanzu yenye damu na vifaa vya kijeshi,
ikiwamo nguo na kitambaa cha kuficha uso. Wananchi walilazimika kutoa
taarifa kwa polisi na hivyo kukamatwa.