WANANCHI WAANDAMANA KISA MINARA YA SIMU ILIYOPO KATIKA KIJIJI CHAO

WANANCHI zaidi ya 300 wa kijiji cha Losimangoi,kata ya Lepurko wilayani Monduli,wameandamana na kutishia kuiteketeza kwa moto Minara mine ya kampuni mbalimbali za simu,iliyopo kijijini kwao,kwa madai kwamba kampuni hizo zimeshindwa kulipa kodi ya ardhi katika kipindi cha miaka nane kijijini hapo.
Wakizungumza kwenye mkutano wa hadhara walioufanyia kando ya Minara hiyo , walisema kijiji chao kiliingia mkataba wa kisheria na kampuni za simu za Tigo,Vodacom,Airtel na Zantel kwa makubaliano ya kulipa kodi ya Ardhi ya kila mwaka ,baada ya kusimika minara hiyo katika kipindi tofauti mwaka 2004.
Mwenyekiti wa kijiji hicho,Lesikari Mollel,alifafanua kuwa baada ya makubaliano hayo kampuni hizo ziliweza kulipa kodi hiyo katika kipindi cha miaka mitano tangu mwaka 2004 hadi 2008 ambapo kampuni zilisitisha ghafla malipo hayo bila kuwepo taarifa yeyote kwa uongozi wa kijiji hicho na kusemekana kwamba zinalipa kwa jeshi la wananchi Tanzania JWTZ wilayani humo.
‘’Tulijaribu kufuatilia lakini mawasiliano na kampuni hizo yalikuwa madogo hadi sasa ambapo wananchi wameamua kuandamana kutaka minara hiyo iondolewe ama waichome moto kwa sababu wahusika hawalipi chochote sisi’’alisema Mollel.
Alisema kipindi hicho kampuni ya Tigo ilikuwa ikilipa kijiji shilingi milioni 3.4 na kampuni za Vodacom,Airtel na Zantel zikilipa shilingi milioni 2.7,fedha ambazo zilitosha kuwasaidia kuendeleza miradi ya maendeleo kijiji hapo, pamoja na kusomesha watoto wasio na uwezo kwa kuwalipia ada .
Mmoja wa wanakijiji hao,Julius Merinyock,alisema kuwa hakuna haja ya kuendelea kukumbutia kampuni ambazo haziwasaidii kwa chochote,kimsingi aliwataka wanakijiji wenzake wainuke wakachome moto minara hiyo .
‘’Kama wato walituona wa nini wacha na sisi tuwaone wa kazi gani ,tuteketeze hii minara ili wajue kuwa hatuitaki iwepo hapa ,miaka nane hawajalipa nani anaweza akavumilia huo ujinga,na leo tunalala hapa tunataka wajitokeze kama hawatakuja tutaenda kuiondoa’’alisema Merinyock.
Naye,mwakilishi wa kampuni ya uwakala inayohudumia minara hiyo kanda ya Kaskazini,Regan Usiri,aliwasihi wananchi hao kuweka hasira kando ili wafikie mwafaka na kampuni husika huku akieleza kuwa atafanya awezavyo ili wahusika wa kampuni hizo waweze kukutana na wananchi hao.
‘’ndugu zangu msijaribu kuharibu miundo mbinu hii kwanza imewarahisishia sana mawasiliano hivi sasa mkitaka kuitana haina haja ya kupuliza pembe mnapigiana simu tu na kukutana ,sasa kama mtaichoma hamwoni kwamba mnarudisha nyuma maendeleo yenu’’alisema .
Hata hivyo aliwaeleza wanakijiji hao kuwa kampuni hizo za simu zimekuwa zikilipa kodi ya ardhi kila mwaka kwa jeshi la wananchi JWTZ wilayani humo na kupatiwa risiti za malipo.
Kwa upande wa afisa mtendaji wa kijiji hicho,Shongon Leswaki aliwasihi wananchi hao kuwa wavumilivu hadi hapo   watakapokutana na kampuni hizo ili kupata ukweli wa malipo ya minara hiyo na sababu za kampuni hizo kusitisha kukilipa kijiji chao.
Aliongeza kuwa kijiji cha Losimangori chenye ukubwa wa eneo la ekeri 14,300 kilisajiriwa kihalali mwaka ,2004 kwa hati ya usajiri namba AR/KIJ/632,kikiwa na wakazi zaidi ya 8500.

Post a Comment

unashauriwa kutoa maoni muda na wakati wowote na kama unahabari yeyote unaruhusiwa kututumia

Previous Post Next Post