Mwenyekiti wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), Rais
Jakaya Kikwete amedokeza kuwa atakayekuwa mgombea wake wa urais baadaye
mwaka huu ni yule ambaye hajajitokeza mpaka sasa.
Akihutubia jana katika sherehe za miaka 38 ya
kuzaliwa kwa chama hicho mjini Songea, mkoani Ruvuma, Rais Kikwete
alisema: “Wapo watu wenye sifa zote za urais lakini hawajitokezi na hata
wakiambiwa kuwa wanaweza husema hawajajiandaa. Hawa ndiyo tunaowahitaji
kwa kuwa wanahitaji kukumbushwa tu.”
Kauli hiyo ya Rais Kikwete inaweza kuwa mwiba
mchungu kwa baadhi ya makada wa CCM ambao kwa muda mrefu wamekuwa
wakipita huku na kule kutafuta uungwaji mkono, huku baadhi yao wakiwa
wamepewa onyo kali kutokana na kushiriki kampeni kabla ya muda na
kushiriki vitendo ambavyo ni kinyume na maadili.
Katika hotuba yake iliyorushwa moja kwa moja na
vituo vitatu vya televisheni, Rais Kikwete alisema chama hicho kitakuwa
na mgombea bora wa urais kwa kuwa upo utaratibu mzuri wa kumpata kwa
kutumia kanuni walizojiwekea. Pia alieleza kwa msisitizo kwamba
kinachokatazwa ni ‘kukiuka kanuni na taratibu.’
“Oktoba tunachagua rais, mimi nataka rais huyo
atoke CCM. Chama kina mfumo wa kumpata mgombea mzuri wa urais na
nawahakikishia kuwa tutakuwa na mgombea bora wa urais na wananchi
hawatanung’unika,” alisema na kuongeza:
“Ushindi ni lazima na nayasema haya kwa bariiidiii na uhakika. Najua kuwa wapinzani wetu hawana chao.”
Rais alieleza kuwa ni lazima CCM ishinde katika
uchaguzi mkuu ujao hasa kwa kuzingatia kuwa imekuwa ikifanya hivyo tangu
mfumo wa vyama vingi uanzishwe, zaidi ya miaka 20 iliyopita.
Alisema ushindi huo haupingiki kwa chama hicho
kutokana na idadi kubwa ya wanachama waliopo na wale wanaotarajiwa
kuandikishwa mwaka huu.
“Tunao wanachama milioni sita mpaka sasa na katibu
mkuu anapanga kutoa kadi nyingine milioni mbili kwa wanachama wapya.
Hiyo itatufanya tuwe na wanachama milioni nane watakaokipigia kura chama
chetu. Hiyo ni idadi kubwa kuliko chama chochote cha siasa kilichopo
hapa nchini. Huo ni mtaji wa kutosha tulionao kabla ya uchaguzi
wenyewe,” alisema.
Hata hivyo, mwenyekiti huyo aliwatahadharisha
wanachama wake kuwa ni lazima wajiandae kukabiliana na upinzani uliopo
na ili kufanikisha hilo, aliwataka wale wote wenye nia kuanza kuwa
karibu na wananchi ili kusikiliza kero walizonazo.
Alisema mwaka huu ni lazima kila kiongozi
ahakikishe anajiweka katika maandalizi kamili; ndani na nje ya chama ili
kukabiliana na changamoto mbalimbali zinazoweza kujitokeza wakati
wowote wa kuelekea katika kinyang’anyiro hicho. “Pamoja na uhalisi wa
ushindi katika uchaguzi ujao, upinzani unaanzia ndani ya chama.
Tushindane kwa nia njema na baada ya hapo tuimarishe umoja miongoni
mwetu ili kuwakabili wapinzani,” aliongeza.
Mfuko wa uchaguzi
Post a Comment
unashauriwa kutoa maoni muda na wakati wowote na kama unahabari yeyote unaruhusiwa kututumia