KATIKA hali isiyo ya
kawaida ,uongozi wa shule ya msingi,Mkoaranga,iliyopo wilayani humo,umesusia msaada
wa mahindi na maharage yaliyotolewa na uongozi wa kijiji kwa ajili ya
matumizi ya chakula kwa wanafunzi shuleni hapo kwa madai kwamba msaada huo
unatoka chama cha upinzani cha chadema na unaweza kuwaletea matatizo ya kufukuzzwa kazi.
Uongozi wa shule hiyo ukiongozwa na mwalimu
mkuu,Samson Kisetu Mbise,ulilazimika kutoweka katika mazingira tata
shuleni hapo, dakika chache baada ya kupata taarifa juu ya kuwasiri kwa msafara wa mwenyekiti
huyo wa kijiji cha Nkoaranga ,Zephania Mwanuo kupitia chama upinzani .
Tukio hilo lilitokea
juzi majira ya saa 7.00 mchana, ambapo Mwenyekiti huyo alifika shuleni
hapo akiwa ameongozana na afisa mtendaji
wake,Aurelian Shio pamoja na wajumbe mbalimbali wa serikali ya kijiji.
''Nimewasiliana
na mwalimu mkuu muda si mrefu akanihakikishia atakuwepo shuleni ,lakini
sasa haonekani ,hata msaidizi wake pia haonekani na mwalimu wa chakula
naye hayupo na kibaya zaidi hakuna taarifa yoyote ya udhuru na simu zao
hazipatikani''.alilalamika mwenyekiti huyo.
Viongozi wa shule hiyo wanaodaiwa
kususia msaada huo kwa madai ya kuhofia kutimuliwa na mwajiri wao ni pamoja na mkuu wa shule hiyo,msaidizi wake,Eliaremisa
Nasary pamoja na mwalimu wa chakula,Kirwa Ndossi.
Mwanuo alisema mbali na
kuleta msaada huo pia ziara hiyo ililenga kutembelea miradi mbalimbali ya shule
na kujionea changamoto ambazo mwalimu mkuu wa shule hiyo alizieleza ili
kuzipatia ufumbuzi wa kuzitatua.
Walimu waliokutwa shuleni hapo nao hawakuwa tayari kutoa ushirikiano wa
kutambua ujio wa msafara wa mwenyekiti huyo,hatua iliyolazimu mwenyekiti huyo
na msafara wake kukaa na magunia hayo yaliyokuwa kwenye gari kwa zaidi ya masaa
matatu wasijue la kufanya .
Baadhi ya wajumbe wa kamati ya shule akiwemo mwenyekiti wa shule,Robert
Kishiri walilaani tukio la kutoweka kwa
uongozi wa shule bila taarifa yoyote na kueleza kuwa kitendo hicho si cha
kiungwana kwakuwa msaada huo haukuwa na chembe yoyote ya kisiasa.
Ilipotimu majira ya saa 9 alasiri mwenyekiti wa shule hiyo alimwendea
mmoja ya walimu katika shule hiyo waliokuwa wamejifungia ofisini na kumsihi
apokee chakula hicho kwa niaba ya mwalimu mkuu ili kuondoa hiyo aibu.
Mwalimu,Anna John Mbise alikubali kupokea msaada huo kwa shingo upande,magunia
11 ya maharage , mahindi gunia 42 na fedha tasilimu shilingi milioni 1.54 kwa
ajili ya malipo ya mpishi,mafuta, kuni na mkaa.
Uchunguzi umebaini kuwa uongozi wa shule hiyo umejawa na hofu ya kupoteza
kazi kutoka kwa waajiri wao ambao hawaungi mkono jitihada za vyama vya upinzani
hali iliyolazimu walimu hao kutoweka.
Msaada huo ni nusu ya ahadi ya kutoa magunia 83 ya mahindi na maharage
gunia 23 yatakayotoshe kutumika kwa mwaka mzima shuleni hapo ,hatua hiyo
imepongezwa na wazazi wa watoto wanaosoma shuleni hapo kuwa ,wataepuka watoto
wao kurudishwa nyumbani kwa kukosa mchango wa kununua chakula.