Rais
wa Tanzania Jakaya Mrisho Kikwete akimkabidhi bendera Kiongozi wa
Batalioni inayoelekea Mashariki mwa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo DRC
kulinda amani
Ofisa wa Jeshi la Ulinzi la Wananchi wa Tanzania (JWTZ), Meja Khatibu Mshindo, aliyekuwa Brigedi ya Kimapigano (FIB), iliyoundwa na Umoja wa Mataifa (MONUSCO), kwenye operesheni za umoja huo, Mashariki mwa Jamhuri ya Kidemorasia ya Kongo (DRC), ameuawa baada ya kujeruhiwa na bomu.
Meja Mshindo alijeruhiwa kufuatia kuangukiwa na bomu linalodaiwa kurushwa na waasi wa kundi la M23 wanaopigana dhidi ya majeshi ya serikali ya DRC mashariki mwa nchi hiyo akiwa na wenzake kwenye eneo lao la ulinzi.
Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa na Kurugenzi ya Habari na Uhusiano ya Makao Makuu ya Jeshi, na kutumwa kwa vyombo vya habari na Msemaji wa JWTZ, Meja Erick Komba, Meja Mshindo alifariki akiwa anapelekwa hospitali na wenzake walioumia, kwa ajili ya matibabu. Hata hivyo hali ya majeruhi wengine inaendelea vizuri.
Hata hivyo, taarifa hiyo haikueleza kama majeruhi wengine ni wanajeshi wa Tanzania ama kutoka nchi nyingine zenye askari Monusco.
Tanzania ni moja ya nchi tatu zinazounda brigedi hiyo ya kimapigano maalum kwa ajili ya kulinda raia na mali zao pamoja na mji wa Goma, ulioko mashariki mwa DRC, dhidi ya wapiganaji wa M23 na makundi mengine ya waasi, wenye silaha. Nchi nyingine ni Malawi na Afrika Kusini.
Kwa takribani wiki nzima sasa, ripoti kutoka kwenye vyombo mbalimbali vya habari vya kimataifa, zimekuwa zikiripoti kuibuka kwa mapiganoya jeshi la serikali ya DRC, linalopigana sambamba na Brigedi ya kimapigano ya UN, dhidi ya waasi wa M23.
UN YATHIBITISHA
Taarifa za kuuawa kwa ofisa huyo wa JWTZ, na mapigano kati ya jeshi la Serikali ya DRC linalosaidiwa na Monusco dhidi ya M23, zilithibitishwa vile vile na Farhan Haq, Msemaji wa UN, jijini New York.
Haq alisema wanajeshi wa Monusco wakitumia helikopta za mashambulizi, waliwashambulia waasi wa M23, ili kuwasukuma nyuma kutoka kwenye maeneo yaliyo jirani na Goma.
Aidha, Shirika la Utangazaji la Uingereza (BBC), lilimnukuu msemaji wa Monusco, Felix Basse, akisema kuwa jeshi lake linapigana likitumia helikopta za mashambulizi na mizinga, sambamba na jeshi la DRC, kwa minajili ya kuzima mashambulizi yanayofanywa na M23 kutoka kwenye milima ya Kibati, iliyo kilometa 15 kaskazini mwa Goma.
FIB inaundwa na jeshi lenye makamanda na wapiganaji 3,000 likiwa na amri ya kuwanyang’anya silaha, na kuzima makundi yote ya waasi wenye silaha katika eneo hilo la mashariki mwa DRC.
Kwa upande wa Kundi la M23, sehemu kubwa ya askari wake wanaundwa na watoro kutoka katika Jeshi la DRC ambao wanadaiwa kupata msaada kutoka Rwanda.
IDADI YA MASHUJAA YAFIKIA 11
Hadi sasa JWTZ imepoteza wanajeshi wake 11, katika operesheni za kulinda amani za Umoja wa Mataifa.
Agosti mwaka jana, Askari watatu wa JWTZ waliokuwa kwenye misheni ya kulinda amani katika jimbo la Darfur nchini Sudan (Unamid), walikufa kutokana na gari lao kusombwa na mafuriko.
Askari hao ni Sajenti Taji Julius Chacha, Koplo Yusuph Said na Private Anthony Daniel.
Walikufa wakiwa kwenye doria ya kawaida kama moja ya majukumu yao wakati wakivuka mto Malawasha, katika kijiji cha Ahamada, baada ya gari lao la deraya kusombwa na maji.
Aidha, Julai 13 mwaka huu, askari saba wa JWTZ katika operesheni hiyo ya Unamid, waliuawa baada ya kuingia kwenye ‘ambush’ wakiwa katika msafara wa kuwasindikiza waangalizi wa amani wa Umoja wa Mataifa.
Walikuwa wakisafiri kutoka eneo la Khor Abeche kwenda Nyala, na waliwekewa ‘ambush’kwenye eneo lililokuwa na mtelemko mkali na lenye utelezi, kufuatia mvua kubwa iliyokuwa imenyesha. Walishambuliwa kwa kushtukizwa na kusababisha kupoteza maisha yao.
Waliouawa ni Sajini Shaibu Othman, Koplo Oswald Chaula, Koplo Mohamed Ally, Koplo Mohamed Chikilizo, Private Fortunatus Msofe, Private Rodney Ndunguru na Private Peter Werema.
Kuuawa kwa Meja Mshindo kunafanya idadi ya wanajeshi wa JWTZ waliopoteza maisha kwenye operesheni za UN, tokea mwaka 2007, JWTZ ilipoanza kuchangia askari huko Darfur, kufikia 11 hadi sasa, wanane wakiwa wameuawa katika makabiliano na adui na wengine kwa ajali ya maji.
CHANZO:
NIPASHE