Arusha. Mazishi ya kifahari yanaandaliwa na familia ya marehemu Erasto
Msuya, huku ikielezwa kuwa jeneza litakalotumika kubeba mwili wake
linafunguka kwa kutumia ‘rimoti’.
Msuya aliyeuawa wiki iliyopita, anazikwa leo huku familia ikitangaza
kutokulipiza kisasi kwa waliohusika, badala yake wamemwachia Mungu.
Kinachovutia katika msiba huo ni jeneza lililobeba mwili wa
mfanyabiashara huyo lililoagizwa Nairobi, la aina yake huku
likifunguliwa kwa kutumia ‘rimoti’.
Jeneza hilo lililoagizwa kutoka Kampuni ya Montezuma & Monalisa
Funeral Home, linafunguliwa kwa kubonyeza kifaa maalumu hata mhusika
anapokuwa mbali.
Hali hiyo ilionekana kuwaacha na mshangao maelfu ya waombolezaji
waliofika kuaga mwili wakati wa ibada iliyofanyika nyumbani kwake, Kwa
Iddi, wilayani Arumeru.
Mfanyabiashara huyo aliyeuawa kwa kumiminiwa risasi zaidi ya 20 na watu
wasiojulikana, anazikwa leo nyumbani kwao eneo la Kairo Mirerani, Wilaya
ya Simanjiro, mkoani Manyara.
Kaka wa marehemu, Israel Msuya, alisema jana kuwa mazishi hayo
yatafanyika makaburi ya familia ya mzee Elisaria Msuya ‘Kikaango’, baba
wa marehemu Erasto.
Kwa mujibu wa Kamati ya Maandalizi ya mazishi hayo inayoongozwa na kaka
mkubwa wa familia ya Msuya, Gady, zaidi ya Sh100 milioni zimepangwa
kugharimia shughuli za maombolezo na mazishi.
Jeneza na gari maalumu la kubebea mwili wa marehemu yameagizwa kutoka
Kampuni ya Montezuma & Monalisa Funeral Home ya Nairobi, Kenya kwa
gharama ya Sh8 milioni.
Chakula, vinywaji, mapambo na magari ya kukodishwa kutoka Arusha kwenda
Mirerani na kurudi yanatarajiwa kugharimu zaidi ya Sh80 milioni.
Katika hatua nyingine, polisi mkoani Arusha imeendelea kuwahoji
wafanyabiashara maarufu wa madini ya Tanzanite wa Mji mdogo wa Mirerani,
wilayani Simanjiro, wakidaiwa kuhusika na kifo hicho.
Habari zilizopatikana jana zinadai mfanyabiashara mmoja kijana ambaye
aliibuka ghafla kuwa tajiri mkubwa kutokana na biashara ya madini ya
Tanzanite, anashikiliwa Arusha kwa mahojiano.
Jana, kwenye viunga vya Mji wa Mirerani watu walitangaziwa kuwa
mfanyabiashara huyo, alikuwa anashikiliwa kwa mahojiano kuhusiana na
kifo hicho.
Hata hivyo, Kamanda wa Polisi wa Mkoa wa Arusha, Liberatus Sabas,
hakupatikana mara moja kuelezea suala hilo kwani simu yake ilipopigwa
ilikuwa haipatikani.
Marehemu ameacha mke na watoto wanne, huku akiacha rasilimali nyingi
ikiwamo jumba la kifahari lililopo Sakina kwa Idd, hoteli maarufu za SG
Resort na Mezza Luna zilizopo Arusha.