Ticker

6/recent/ticker-posts

WAIOMBA SEREKALI KUWAFUNGULIA MIGODI ILIYOFUNGWA

Na Woinde Shizza,Manyara
Wachimbaji madini wa migodi minne ya Tanzanite Mji mdogo wa Mirerani
Wilayani Simanjiro Mkoani Manyara, ambayo imesimamishwa kufanya kazi
wameiomba Serikali kuifungulia, ili waendelee na shughuli zao za
uchimbaji.



Wachimbaji hao waliogoma kutaja majina yao walisema tangu wasimamishwe
kazi Julai 23 mwaka huu, baada ya mchimbaji wa TanzaniteOne kuuawa kwa
kupigwa risasi na mtu asiyejulikana, haijakaguliwa kama Serikali
ilivyoagiza.



Wachimbaji hao walisema migodi hiyo yenye kutoa ajira kwa wachimbaji
zaidi ya 2,000 mbali na familia zao, hivi sasa wameathirika kwani
wanaishi bila kufanya kazi, hivyo wanapata wakati mgumu kupata fedha
za kujikimu.



Pia walisikitishwa na kitendo cha migodi yao kusimamishwa kazi, huku
migodi ya kampuni ya TanzaniteOne wanayopakana nayo ikiendelea kufanya
kazi na kuwapa mshangao kwa kukosekana usawa katika uchimbaji madini.



“Tunaomba Serikali ifanye uchunguzi wao kwa haraka na busara ili sisi
tuweze kuendelea na kazi zetu, kwani hata Joseph Mwakipesile Chusa
wamemshikilia kwa shinikizo tu la wachimbaji wa kampuni hiyo, hausiki
na lolote,” walisema.



Walidai kuwa baadhi ya wafanyakazi wa kampuni hiyo huwa wanashirikiana
na wachimbaji wasio rasmi katika kufanya kazi kwenye kampuni hiyo na
pindi wakidhulumiana ndiyo hutokea matatizo na kusingizia wachimbaji
wadogo.



Hata hivyo, Katibu wa chama cha wachimbaji madini mkoa wa Manyara
(Marema) Tawi la Mirerani, Abubakary Madiwa alikiri kupata barua  ya
wachimbaji hao kulalamika kufungiwa migodi hiyo kwa muda mrefu.



“Tutafuatilia suala hili kwani hata sisi tunatambua kuwa wachimbaji
hao wakikaa bure bila kufanya kazi wanaweza kujiingiza kwenye vitendo
viovu na pia ni hasara kwa wamiliki wanaoendelea kuwahudumia,” alisema
Madiwa.

Post a Comment

0 Comments