Miezi sita baada ya kujiuzulu, Papa Benedict XVI, amefungua mdomo na kueleza sababu za kufikia uamuzi huo wa kushangaza.
Jana, vyombo vya habari vilimkariri Papa Mstaafu Benedict akimweleza mgeni wake kuwa aliitwa na Mungu kwa miujiza.
Kiongozi huyo ambaye alishangaza watu kwa uamuzi
huo wa Februari 8, mwaka huu, hata hivyo alisema sauti ya Mungu imejibu
kupitia kwa mfuasi wake, Papa Francis.
Papa Benedict alitangaza uamuzi wa kujiuzulu Februari 11, maelezo yake yalielekeza katika afya yake.
Alisema nguvu zake zilikuwa zimepungua kiasi cha kutokuweza kumudu majukumu yake ipasavyo.
Alisema, “Mungu aliniambia ‘niondoke,’ nami
nikatimiza wajibu huo bila kusita,” alisema Papa Benedict ambaye amekuwa
kiongozi wa kwanza kufikia uamuzi huo baada ya miaka 600 ya Kanisa
Katoliki. Alisema tangu wakati huo ameishi maisha ya sala.
Mkongwe huyo mwenye umri wa miaka 86 alisema
ameshuhudia maono ya Mungu kwa miezi kadhaa huku akisikia sauti na tamaa
ya kuendelea kuwa karibu naye (Mungu).
Papa Benedict, hata hivyo alisema Mungu amembariki
na kumwezesha kuuona utukufu wake kupitia kwa Papa Francis, akielewa
kwa nini alitakiwa kuondoka mapema kwa kuitika sauti na utashi wa Mungu.
Shirika la Habari la Kikatoliki (Zenit), hata hivyo halikueleza ni nani aliyekuwa akizungumza na Papa Benedict.
Hata hivyo, kauli hiyo ya Papa Benedict imeungwa mkono na vyanzo vya kuaminika kutoka Vatican.
“Ni ripoti ya kuaminika, ina usahihi, inaeleza
mchakato wa kiroho ambao Papa Benedict aliupitia kabla ya kujiuzulu,
vyanzo hivyo vililiambia gazeti la The Times.
Wachunguzi wa mambo wamekuwa wakieleza kuwa Papa
Benedict alikatishwa tamaa na kuvuja kwa siri za mawasiliano yake
binafsi na msaidizi wake .