Sehemu ya waandishi wa habari wakiwa kwenye mkutano na Katibu Mkuu wa EAC,Dk Richard Sezibera leo
Katibu Mkuu wa Jumuiya ya
Afrika Mashariki,Balozi Dk Richard Sezibera amesema mgogoro kati ya Rais
wa Tanzania,Dk Jakaya Mrisho Kikwete na mwenzake wa Rwanda,Paul Kagame
hauwezi kuathiri kwa kiwango cha kuvunja jumuiya hiyo japo sio afya
kwa juhudi za mtangamano.
Amesema jitihada za kuutatua mgogoro zinafanywa na EAC pasipo kutaka
kuingiliwa na vyombo vya habari na kua njia pekee ya kuumaliza ni
kwanjia ya kidiplomasia.
“Tunaendelea na mashauriano ambayo hatujapenda vyombo vya habari
kuingilia kwa sasa,tunaamini njia sahihi ni njia ya kidiplomasia zaidi”
Hata hivyo alikanusha taarifa zilizoenea kuwa wafanyakazi wa Tanzania
na Rwanda wanaofanya kazi EAC wamekuwa hawasemeshani kutokana na
mgogoro huo.
Dr Sezibera akizungumzia raia wa kigeni walioamriwa kuondoka mkoani
Kagera ,alisema anaamini kila nchi ina utaratibu wake lakini hakuna
sababu ya kuwaita raia wa Afrika Mashariki wahamiaji haramu kwani
wananchi wa eneo hili ni wamoja.
Alisema Kanda ya Afrika Mashariki inakabiliwa
na migogoro mikubwa ukilinganisha na maeneo mengine yakiwamo makundi
yaliyofanya mauji ya kimbali na mengine kama kikundi cha FNL cha Burundi
na mengine jambo linalohatarisha usalama kwa ujumla.
Wakati Tanzania ikisema kuwa iko tayari
kukaa meza moja na jirani yake Rwanda kumaliza hali ya uhasama iliyoanza
kujitokeza katika siku za hivi karibuni, Katibu Mkuu wa Sekretarieti ya
Jumuiya ya Afrika Mashariki, Dk Richard Sezibera amesema jitihada za
kidipolomasia zinafanyika kutatua tofauti hizo za kimawazo.Bila kutaja
taasisi wala wanaohusika katika jitihada hizo za kidiplomasia, Dk
Sezibera aliwaambia waandishi wa habari jijini Arusha jana kuwa jitihada
hizo zinafanyika kimya kimya bila kushirikisha vyombo vya habari
"Migongano na tofauti za kimtazamo miongoni mwa viongozi wakuu wa nchi
wanachama wa EAC ni jambo lisilo la afya kwa Jumuiya na linastahili
kushughulikiwa kidiplomasia," alisema Dk Sezibera.
Akizungumza kwa tahadhari kubwa kukwepa
kuingia kwa undani kuhusu suala hilo, Katibu Mkuu huyo alisema inafaa
kila linalowezekana lifanyike kutatua mgongano wowote unaotokea kati ya
viongozi wakuu.
Mjini Dar es Salaam, Waziri wa Mambo ya
Nje na Ushirikiano wa Kimataifa, Benard Membe naye alisema katika
mahojiano kuwa iwapo Rwanda itaomba kukutana na Tanzania kwa ajili ya
kumaliza mzozo huo Serikali itakuwa tayari kutoa ushirikiano.
"Tanzania tunaona kuwa hii itakuwa njia
ya busara zaidi kumaliza tofauti zetu kwa njia ya mazungumzo badala ya
kuendelea kuishi kwa uhasama" alisema Membe na kwamba hali ya ujirani
mwema na tofauti zetu tuzimalize kwa njia ya mazungumzo."
Waziri Membe alisema siyo jambo la busara
kuacha mzozo huo ukakaamuliwa na mataifa ya nje ili hali nchi zenyewe
bado zinafursa nzuri ya kukaa mezani na kujadiliana namna ya kutafutia
ufumbuzi mzozo huo.
Uhusiano wa Tanzania na Rwanda unatajwa
kuwa katika wakati mgumu kutokana na kauli za majibizano baina ya
viongozi wa pande zote mbili. Hivi karibuni Rais Jakaya Kikwete aliisihi
Rwanda kutotoa kauli za kejeli kwani kwa kufanya hivyo kunaweza
kuhatarisha uhusiano uliodumu kwa muda mrefu .
Hata hivyo, Dk Sezibera alisema tofauti
na migongano kati ya viongozi haiwezi kuathiri wala kuvunja Jumuiya ya
sasa ya Afrika Mashariki kama ilivyotokea kwenye Jumuiya ya awali mwaka
1977 kutokana utofauti wa muundo na misingi ya Jumuiya ya sasa.
"Jambo lililo dhahiri ni kwamba tofauti
za kimtazamo kati ya viongozi wa nchi wanachama (Kikwete na Kagame),
haziwezi kuhatarisha uhai wa Jumuiya ya Afrika Mashairiki kwa sababu
muungano huu umejengwa katika muundo na misingi imara tofauti na ule
(jumuiya) wa zamani," alisema Dk Sezibera
kwa hisani ya rweyumamu info blog
|