WAKATI Rais Jakaya Kikwete akidaiwa kukalia orodha ya mtandao wa
vigogo wanaojihusisha na biashara ya dawa za kulevya, Kamanda wa Polisi
wa Viwanja vya Ndege nchini, Deusdedit Katto, amewataka wanaowafahamu
watuhumiwa hao watoe taarifa.
Katika mazungumzo yake na kituo cha televisheni cha Channel Ten juzi,
Katto alisema hawafahamu vigogo hao wanaotuhumiwa na kwamba yeyote
mwenye ushahidi akatoe taarifa.
“Wakati mwingine tunasema tu, kama tuna ushahidi kuhusu hilo utolewe.
Mimi nalisikia neno hilo la vigogo hata kabla sijaja hapa,” alisema
Katto alipotakiwa kufafanua kuhusu uuzaji wa dawa hizo kuhusisha mtandao
mkubwa.
Alisema hilo ni tatizo kubwa duniani na kwamba hakuna serikali yoyote ambayo inacheza nalo.
Alisema wanapambana na suala hilo kwa namna mbalimbali na kudai kuwa
kuna baadhi ya nchi ndogo wafanyabiashara hiyo wamekuwa wakishindana na
serikali zao.
Kuhusu uteketezaji wa dawa hizo kufanyika kwa siri, Katto alisema si
kweli kwani taratibu zinafuatwa kwa kuwashirikisha watu wengi.
“Kuna vyombo vinatajwa lazima viwepo wakati wa kuteketeza, mfano jaji
aliyesikiliza kesi, mawakili wa serikali na wale wa utetezi, Mkemia Mkuu
wa Serikali ili athibitishe kama zilizoteketezwa ni dawa za kulevya,”
alisema.