HIKI NDO KILICHOMSUMBUA MCHUKUNGAJI KOLOLA

Askofu Mkuu wa Kanisa la Evangelistic Assemblies of God nchini (EAGT), Dk. Moses Kulola, amefariki dunia.
Akizungumza na NIPASHE  kwa njia ya simu jana mtoto wake, William Kulola, alisema kuwa  baba yake alifariki jana saa 5:00 asubuhi katika Hospitali ya Ami (African Medical Investments) iliyoko Masaki jijini Dar es Salaam.

Alisema mwili wake ulihamishwa hospitalini hapo  na kupelekwa  Hospitali ya Profesa Kairuki iliyoko Mikocheni jijini humo.

Kwa mujibu wa habari kutoka ndani ya familia ya Dk. Kulola, mwili huo utaondolewa hospitalini hapo na kupelekwa Kanisa la EAGT lililokoTemeke kwa ajili ya kuagwa kesho saa 2:00 asubuhi.

“Wakazi wote wa Dar es Salaam wanaombwa kufika katika Kanisa la EAGT Temeke, Jumamosi (kesho) saa mbili asubuhi kwa ajili ya kuuaga mwili wa marehemu,” alisema William na kuongeza:

“Baada ya kuagwa, mwili wa baba yake unatarajia kuwasili  Mwanza  Jumapili  wiki hii kwa ajili ya mazishi siku ya Jumatano wiki ijayo.”

Naye mjukuu wa marehemu, Naomi Zegezege, akithibitisha kifo hicho alisema: “Ni kweli amefariki siyo muda mrefu katika Hospitali ya Ami Masaki, nenda katika hospitali hiyo utakutana na familia yote watakueleza. Alipelekwa India kwa ajili ya matibabu, lakini alirudishwa baada ya kufanyiwa upasuaji.”

Naomi aliongeza kuwa: “Kwa kuwa huyu alikuwa ni mtu mkubwa sana, naamini kuwa, kabla ya mwili wake kusafirishwa kwenda Mwanza kwa ajili ya mazishi, utaagwa kwanza hapa Dar es Salaam.”

Uongozi wa Hospitali ya Ami haukuwa tayari kufafanua kuhusiana na ugonjwa uliosababisha kifo cha kiongozi huyo mashuhuri wa dini nchini kwa maelezo kuwa wenye mamlaka ya kufanya hivyo ni familia.

Kwa mujibu wa taarifa zilizotolewa na mtoto wake ambaye pia ni Mwinjilisti wa Kimataifa wa kanisa hilo, Dk. Daniel Kulola, kupitia mitandao  ya kijamii jana,  baba yao huyo alifariki dunia kutokana na kwa shinikizo la damu.

Katika taarifa yake kupitia mtandao wake wa Facebook, Dk. Danieli   mbaye pia ni Mchungaji wa kanisa hilo eneo la Lumala Mpya, alisema: “Watu wa  Mungu salam, nina salamu za majonzi, baba yangu Kulola, amefariki dunia muda si mrefu.”

Kabla ya kufikwa na kifo hicho, Askofu Kulola, ambaye alizaliwa mwaka 1928, amekuwa akisumbuliwa na udhaifu wa  mguu mmoja kwa muda mrefu uliosababisha kupelekwa India kwa matibabu takribani miezi miwili iliyopita.

FLORA MBASHA AZIMIA
Baada ya kusikia habari hizo za kifo, mwimbaji  maarufu wa nyimbo za injili nchini ambaye pia ni mjukuu mwingine wa Dk. Kulola, Flora Mbasha, alizimia na kisha kukimbizwa hospitali.

Hata hivyo, habari zilizolifikia gazeti hili kabla ya kwenda mitamboni, Flora, alikuwa ameruhusiwa na anaendelea vizuri.

Kabla ya kufikwa na kifo hicho, Dk. Kulola, aliwahi kusumbuliwa na matatizo ya mguu kusuguana kutokana na safari mbalimbali za kumtumikia Mungu hata hivyo, alitibiwa na afya yake kuimarika.

Hivi karibuni kabla ya kupelekwa India, Dk. Kulola, alilazwa katika Hospitali ya Rufaa ya Bugando, jijini Mwanza kwa matibabu kutokana na kusumbuliwa na matatizo ya kiafya na kwamba Agosti 22, mwaka huu aliruhusiwa kutoka hospitalini hapo.

Habari zaidi ambazo NIPASHE ilizipata jana zinasema kuwa Dk. Kulola hadi mauti yanamkuta  alikuwa anasumbuliwa na matatizo ya kuvimba moyo na mapafu.

JK AMLILIA
Rais Mrisho Kikwete amesema ameshtushwa na kuhuzunishwa na taarifa za kifo cha Askofu Kulola.
Rais kikwete ameelezea mshtuko na huzuni yake katika salamu za rambirambi alizomtumia Katibu Mkuu wa Kanisa hilo, Brown Mwakipesile, kufuatia kifo hicho.

“Nimeshtushwa, nimesikitishwa na kuhuzunishwa sana na taarifa za kifo cha Mtumishi wa Mungu wa muda mrefu na Askofu Mkuu wa EAGT, Marehemu Moses Kulola kutokana na maradhi yaliyomfanya wakati fulani apelekwe hadi India kupatiwa matibabu,” alisema Rais Kikwete.

Alisema alimfahamu Askofu Kulola kwa miaka mingi wakati wa enzi za uhai wake, kama Mtumishi Hodari wa Kiroho aliyejitoa vilivyo kuwahudumia waumini wa kanisa lake ambalo mahubiri yake yametoa mchango mkubwa katika kuimarisha imani za Waumini wake na kusaidia kwa kiasi kikubwa katika kudumisha amani na utulivu wa nchi yetu.

Alisema kifo cha Kulola kimeacha pengo kubwa siyo tu kwa Waumini wa kanisa lake, bali pia miongoni mwa wapenda amani kote nchini na  duniani kwa vile enzi za uhai wake,  aliweza kufikisha ujumbe muhimu wa kiimani kupitia mahubiri yake kwa watu wa mataifa mbalimbali ndani na nje ya  Bara la Afrika.

Kulola amecha mjane na watoto saba. Mungu roho yake mahali pema pepon. Amina.
CHANZO: NIPASHE

Post a Comment

unashauriwa kutoa maoni muda na wakati wowote na kama unahabari yeyote unaruhusiwa kututumia

Previous Post Next Post