Mwandishi Mwandamizi wa New habari 2066, Ltd, Mwani Nyangassa (wa pili
kulia) akionyesha uwezo wake wa kusebeneka na baadhi ya wanahabari
wakati wa Tamasha la Waandishi wa Habari lililofanyika kwenye Ufukwe wa
Cine Club, Jijini Dar es salaam mwaka jana. Picha na Maktaba.
Baadhi ya wanahabari wakishindana katika mchezo wa kuvuta kamba.
*****************************************
Mwandishi wetu, Arusha
TAMASHA la nane la vyombo vya habari mkoa wa Arusha, linatarajiwa
kufanyika Septemba 8, 2013 katika viwanja vya General tyre Arusha na
kushirikisha waandishi kutoka jijini Dar es Salaam, Tanga, Kilimanjaro
na mkoa wa Manyara.
Tamasha hili, ambalo hufanyika kila mwaka, limedhaminiwa na kampuni ya bia nchini(TBL).
Akizungumza na waandishi wa habari jana, Katibu wa Chama cha Waandishi
wa habari za michezo mkoa wa Arusha(TASWA) Mussa Juma, alisema zaidi ya
waandishi wa habari na wadau wa habari 500 wanatarajiwa kushiriki
katika Tamasha hilo.
Juma alisema kwa upande wa michezo timu ambazo zitashiriki ni TASWA FC
kutoka jijini Dar es Salaam, TASWA Arusha, Radio Sunrise, Radio 5, Radio
Triple A, Arusha One Radio na Chuo cha Uandishi wa habari Arusha ambao
ndio mabingwa watetezi.
Alisema pia kutakuwa na timu ambazo zimealikwa ambazo ni timu ya TBL
Arusha ambao ndio wadhamini wakuu wa Tamasha hilo, timu ya Wazee
Klabu,Kitambi Noma, Timu ya Pepsi na timu ya NSSF Arusha.
Juma alisema katika tamasha hilo, ambalo huandaliwa na TASWA na kampuni
ya Ms Unique, kutakuwa na michezo ya soka, kuvuta kamba, kukimbiza kuku,
mpira wa mikono na mbio za magunia.
Alisema Septemba 7 bonanza hilo, litatanguliwa na semina ya siku moja
kwa waandishi wa habari mkoa wa Arusha kuhusiana na sheria za michezo,
masuala ya afya na jinsi ya kutumia michezo katika kutangaza utalii.