SIPITEK ACHAGULIWA KUWA MAKAMU MWENYEKITI SIMANJIRO

Makamu Mwenyekiti wa Halmashauri ya Wilaya ya Simanjiro Mkoani Manyara, Jackson Sipitek, amefanikiwa kurudia nafasi hiyo, baada ya Baraza la Madiwani wa wilaya hiyo kumchagua tena kuendelea na uongozi wake.

Sipitek alichaguliwa na madiwani hao juzi, baada ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) wilayani humo, kupitisha jina lake na kulikata jina la diwani wa kata ya Shambarai, Alais Edward ambaye naye aliomba kugombea nafasi hiyo.

Makamu Mwenyekiti huyo Sipitek, ambaye pia ni diwani wa kata ya Langai aliweza kuchaguliwa tena kushika nafasi hiyo, kwa kupata kura zote 21 za madiwani waliokuwepo kwenye kikao hicho.

Naye, diwani wa kata ya Naberera Sumleck Ole Sendeka, akichaguliwa kuwa Mwenyekiti wa kamati ya Elimu, Afya Maji na diwani wa Orkesumet Naftal Ole Peshut, alichaguliwa kuwa Mwenyekiti wa kamati ya Uchumi, Ujenzi na Mazingira.

Akizungumza baada ya kuchaguliwa tena kushika nafasi hiyo, Sipitek alisema ataitumia nafasi hiyo kwa kuwaunganisha madiwani wote wa halmashauri ya wilaya hiyo kwa ajili ya kuwatumikia wananchi.

“Napenda kuwashukuru waheshimiwa madiwani wote kwa imani yao kubwa mlioionyesha kwangu, hadi kunirudisha tena kuendelea kuishika nafasi hii ya Makamu Mwenyekiti wa halmashauri yetu,” alisema Sipitek.

Alisema ataendelea na uongozi wake makini na zaidi ataondoa makundi wilayani humo na atahakikisha miradi ya maendeleo inagawanywa sawa kwa kila kata bila kubagua na kudhani kuwa, kuna kata bora zaidi ya nyingine.

“Kata zote ni sawa sawa katika wilaya yetu, hivyo hakuna kata ambayo ni bora zaidi ya nyingine au diwani bora kuliko mwingine, nitasimamia hayo ili kuhakikisha maendeleo yanaendelea kupatikana Simanjiro,” alisema Sipitek.

Post a Comment

unashauriwa kutoa maoni muda na wakati wowote na kama unahabari yeyote unaruhusiwa kututumia

Previous Post Next Post