Baada ya timu
ya soka ya Simba SC ya jijini Dar es salaam jana kucheza ligi kuu ya Vodacom na
Oljoro JKT jijini Arusha, leo wanatarajia kutembelea machimbo ya madini ya
Tanzanite ya mji mdogo wa Mirerani wilayani Simanjiro Manyara.
Akizungumza
na gazeti hili, Ofisa mahusiano wa kampuni ya TanzaniteOne, Khalifan Hayeshi
alisema timu ya Simba baada ya kufika kwenye machimbo hayo itatembelea na
kujionea namna shughuli za uchimbaji zinavyoendelea.
“Ni ziara ya
kutalii kwenye eneo letu na lengo ni kufahamu namna madini ya Tanzanite
yanavyochimbwa na kupatikana hivyo tunatarajia leo alhamisi watakuwa hapa
kwetu TanzaniteOne,” alisema Hayeshi.
Naye,
Mkurugenzi wa timu ya soka ya Tanzanite FC, Jofrey Nyigu (Mnyalu) alisema baada
ya timu ya Simba kutoka kutembelea migodi ya madini ya kampuni ya TanzaniteOne
watafika mji mdogo wa Mirerani kuiona timu yake.
“Pia watafanya
mazoezi na timu yetu jioni, kabla ya kwenda kuweka mwili vizuri kwenye sehemu
mpya ya Nicks Barbershop hapa mji mdogo wa Mirerani kisha wataondoka kwenda
jijini Dar es salaam,” alisema Nyigu.
Kwa upande
wake, Makamu Mwenyekiti wa timu ya Simba Joseph Itangare (mzee Kinesi)
alithibitisha timu yake kufanya ziara ya kutembelea mji mdogo wa Mirerani
mkoani Manyara.
“Baada ya leo
(jana) kucheza mechi yetu na JKT Oljoro tunatarajia kesho (leo) kutembelea
machimbo ya madini ya Tanzanite na kufanya utalii wa ndani mji mdogo wa Mirerani
kabla ya kurudi jijini Dar es salaam,” alisema.