MFANYABIASHARA
maarufu wa madini aina ya tanzanite jijini Arusha, Erasto Msuya, ameuawa
kikatili kwa kumiminiwa risasi takriban kumi karibu na Uwanja wa Ndege wa
Kimataifa wa Kilimanjaro (KIA).
Tukio
hilo lililogubikwa na utata wa hali ya juu kutokana na mazingira yake,
lilitokea jana mchana eneo la Mijoholoni, wilayani Hai, wakati marehemu akiwa
njiani kutokea Arusha.
Habari
zilizopatikana jana na kuthibitishwa na Kamanda wa Polisi wa Mkoa wa Kilimanjaro,
Robert Boaz, zilisema kuwa mfanyabiashara huyo bilionea alikutwa na mauti hayo
akiwa na gari lake la kifahari aina ya Range Rover lenye namba za usajili
T 800 CKF.
Hata
hivyo, Kamanda Boaz hakuweza kutoa taarifa zaidi juu ya mauaji hayo
kutokana na kile alichodai alikuwa akielekea eneo la tukio na kuahidi kutoa
taarifa mara baada ya kurejea kutoka eneo hilo la tukio.
Taarifa
zaidi zilizolifikia gazeti hili zilidai kuwa Msuya alipigwa risasi na watu
wawili waliokuwa wamepanda pikipiki na kupita eneo alilokuwa amesimama nje ya
gari lake akizungumza kwa simu.
Baadhi
ya marafiki zake jijini Arusha waliokuwa naye muda mfupi kabla ya tukio hilo
walidai kuwa alipigiwa simu akiitwa eneo hilo kwa ajili ya kumuuzia madini.
Katika
hali inayoacha maswali kuhusu tukio hilo, wauaji hao hawakuchukua kitu chochote
kuanzia gari, fedha sh milioni 100 zilizokuwa ndani, simu za mkononi pamoja na
ipad.
Chanzo
chetu cha habari kilidokeza kuwa tukio hilo huenda limepangwa ili kuzima
vuguvugu la tuhuma za mauaji ya mchimbaji mmoja aliyeuawa hivi karibuni kwenye
machimbo ya Mererani.
Kwa
mujibu wa watoa habari walioomba kuhifadhiwa majina yao, sakata la kesi hiyo
limekuwa na utata mkubwa kutokana na Jeshi la Polisi mkoani Arusha kutaka
kumkumbatia mtuhumiwa wa mauaji hayo, kwa kutomfikisha mahakamani.
Marehemu
Msuya anatajwa kama mmoja wa wachimbaji waliokuwa mstari wa mbele kuwashinikiza
polisi kuhakikisha kesi hiyo inafikishwa mahakamani ili haki itendeke kwa
wahusika kuchukuliwa hatua za kisheria.
Tukio
hilo limeanza kuibua hofu miongoni mwa wananchi wa kawaida na wafanyabiashara
juu ya kurejea kwa matukio ya ujambazi wa kutumia silaha uliokuwa umepoa kwa
muda katika mikoa ya Kilimanjaro na Arusha.
Baadhi
ya wafanyabiashara waliozungumza na Tanzania Dama jana, wamedai kuwa tukio hilo
bado limegubikwa na utata kutokana na mazingira yake, kwani gari la marehemu
lilikutwa limeegeshwa pembeni mwa barabara kuu ya Arusha - Moshi kana kwamba
kulikuwa na mazungumzo baina ya marehemu na wauaji.