KARIM BENZEMA ANG'ARA REAL MADRID IKIIUA ATHLETIC BILBAO 5-1... LIONEL MESSI ATUPIA MAWILI KUIPA BARCELONA USHINDI WA 3-1... MESSI SASA ABAKIZA MAGOLI SABA TU KUFIKIA REKODI YA MIAKA YOTE YA MABAO KWA MWAKA WA KALENDA INAYOSHIKILIWA NA MJERUMANI GERD MULLER TANGU MWAKA 1972...






MADRID, Hispania

Barcelona walijichimbia kileleni mwa msimamo wa La Liga, Ligi Kuu ya Hispania kwa tofauti ya pointi sita dhidi ya Atletico Madrid wakati Lionel Messi alipofunga magoli mawili kwa mara ya saba msimu huu na kutengeneza jingine lililofungwa na Alex Song kwa mara ya kwanza tangu asajiliwe na klabu hiyo katika ushindi wao wa 3-1 dhidi ya Real Zaragoza jana (Novemba 17, 2012).

Mwanasoka Bora wa Dunia, Messi aliongeza idadi ya magoli yake msimu huu hadi kufikia 17 baada ya kufunga mabao safi wakati Barca ambayo haijafungwa katika La Liga msimu huu ikifikisha pointi 34 kutokana na mechi 12.

Atletico wana pointi 28 na leo Jumapili (Novemba 18, 2012) watacheza dhidi ya Granada, wakati Real Madrid inayokamata nafasi ya tatu ikipunguza tofauti ya pointi baina yao na Atletico kuwa pointi mbili baada ya kushinda nyumbani 5-1 dhidi ya Athletic Bilbao.

Baada ya goli la mapema la kujifunga la Jon Aurtenetxe, Karim Benzema, Sergio Ramos, Mesut Ozil na Sami Khedira wakaongeza mengine kwa kikosi cha kocha Jose Mourinho kikiendelea kuimarika baada ya kuanza msimu wka kusuasua ambapo sasa wameshinda mechi saba katika mechi nane zilizopita.

Real sasa wamefunga magoli 19 dhidi ya Bilbao katika mechi zao zilizopita za La Liga kwenye Uwanja wa Bernabeu na tukio la kushangaza lilikuwa ni kwa straika Cristiano Ronaldo kushindwa kuongeza idadi ya mabao 12 aliyo nayo katika La Liga msimu huu baada ya kutofunga jana.

Straika huyo wa zamani wa Manchester United alirejea uwanjani akiwa na jeraha la juu ya jicho aliloumia katika mechi iliyopita ya La Liga waliyoshinda 2-1 dhidi ya Levante.

Messi sasa amefikisha magoli 78 katika mwaka wa kalenda wa 2012 kwa klabu yake (magoli 66) na kwa nchi yake ya Argentina (magoli 12) na anaikaribia kwa kasi rekodi inayoshikiliwa na Mjerumani Gerd Muller aliyefunga magoli 85 mwaka 1972.

Ushindi wa jana wa Barca pia unamaanisha kuwa kocha Tito Vilanova, aliyerithi mikoba ya Pep Guardiola mwishoni mwa msimu uliopita, amekuwa kocha wa kwanza kuiongoza timu kupata ushindi wa mechi 11 katika mechi 12 za ufunguzi wa La Liga tangu kocha Radomir Antic afanye hivyo wakati akiwa na Real Madrid msimu wa 1991-92.

MATOKEO MECHI ZA LA LIGA JANA JUMAMOSI (NOV. 17, 2012)

Barcelona    3 Real Zaragoza   1 
Osasuna      0 Malaga              0 
Real Madrid 5 Athletic Bilbao    1 
Valencia       2 Espanyol           1 

MATOKEO MECHI ZA SERIE A ZILIZOCHEZWA JANA JUMAMOSI (NOV. 17, 2012)

Juventus 0 Lazio      0 
Napoli     2 AC Milan 2 

Post a Comment

unashauriwa kutoa maoni muda na wakati wowote na kama unahabari yeyote unaruhusiwa kututumia

Previous Post Next Post