BARAZA la Madiwani wa Halmashauri ya Wilaya ya
Simanjiro Mkoani Manyara limemuagiza mkaguzi wa ndani akakague ujenzi wa shule
ya sekondari Songambele kata ya Mirerani kutokana na mahesabu ya ujenzi wake
kutowaridhisha.
Akisoma azimio ambalo liliungwa mkono na madiwani
hao,Mwenyekiti wa kamati ya Elimu,Afya
na Maji,Sumleck Ole Sendeka alisema mkaguzi huyo aende akakague shule hiyo
kwani halmashauri hiyo imewekeza fedha nyingi.
“Hatuwezi kukubali fedha za wananchi zipotee
hivi hivi kwani wilaya ilitoa fedha na mabati kwa ajili ya ujenzi wa shule hiyo
ya sekondari Songambele ambayo inategemea kupokea wanafunzi mwakani,” alisema
Sumleck.
Hali hiyo ilijitokeza baada ya Ofisa mtendaji
wa kata hiyo,Stephen Wenga kusoma taarifa na kudai kuwa shule hiyo imefikia
kwenye mtambaa panya na hajakabidhiwa mahesabu na aliyekuwa mtendaji wa kata
hiyo,Valentine Tesha.
Hata hivyo,Sumleck na Baraza hilo lilimpongeza
diwani wa kata ya Mirerani,Justin Nyari kutokana na kitendo cha kutumia fedha
zake na kujenga madarasa mawili ya shule ya msingi Tanzanite iliyopo mtaa wa
Songambele.
Naye,Ofisa mtendaji wa kata ya Endiamtu,Edmund
Tibiita alisema kata hiyo imetekeleza miradi tisa ya maendeleo ikiwemo ujenzi
wa madarasa ya shule ya Endiamtu,wodi ya kina mama,kusambaza maji na ujenzi wa barabara.
Tibiita alisema kuwa diwani wa kata hiyo,Lucas
Zacharia alijitolea fedha zake binafsi sh4 milioni kwa ajili ya ujenzi wa
madarasa ya shule ya msingi Jitegemee,jambo ambalo lilipongezwa na Baraza hilo
la madiwani.
Kwa upande wake,Ofisa mtendaji wa kata ya
Orkesumet,Shaaban Mkopi alitaja baadhi ya miradi iliyotekelezwa ni pamoja na ukarabati wa majengo ya
sekondari,zahanati na mradi wa uchomeaji orkesumet.
Mkopi alitaja baadhi ya miradi mingine kuwa ni
ununuzi wa wa vifaa vya maabara ya Veta-Center,ukarabati wa mtandao wa maji
vitongoji vya Jitegemee na madukani pamoja na uendelezaji wa nyumba za
walimu.
Post a Comment
unashauriwa kutoa maoni muda na wakati wowote na kama unahabari yeyote unaruhusiwa kututumia