BREAKING NEWS

Tuesday, November 20, 2012

TAASISI ZA FEDHA ZASHAURIWA KUPELEKA HUDUMA VIJIJINI

TAASISI za Fedha zimeshauriwa kuhakikisha kuwa wanapeleka huduma zao
hata Vijijini kwa kuwa asilimia kubwa ya wananchi wa Vijijini hawana
uelewa wa kutosha juu ya matumizi ya Taasisi hizo za fedha hali ambayo
nayo inachangia kukithiri kwa changamoto mbalimbali zikiwemo za
matumizi mabaya ya fedha na mali



Kauli hiyo imetolewa mjini hapa na Mkurugenzi wa Halmashauri ya Meru
Trasias Kagenzi wakati alipokuwa akiongea na Walimu mbalimbali ambao
ni wadau wa Benki ya NMB katika Siku ya Mwalimu iliyoazimishwa na
Benki hiyo.



Kagenzi alisema kuwa kwa sasa Taasisi nyingi sana za fedha zimejikita
zaidi kwenye maeneo ya Mijini huku kwa upande wa Vijijini wakiwa
wamesahulika ingawaje kijijini ndiko kwenye fursa nyingi sana za Fedha
ambazo zimesahulika sana hali ambayo nayo inachangia sana Umaskini.



Aliongeza kuwa Taasisi hizo za Fedha zinatakiwa kubadilisha na
kuimarisha mifumo zaidi hasa Vijijini ambapo kuna fursa nyingi lakini
hazitambuliki kutokana na wananchi kushindwa kujimudu kimaisha lakini
kama Taasisi za Fedha zingejikita zaidi basi hata uchumi wa vijiji
pamoja na Mikoa ingeweza kuimarika sana na kufanya hata kiwango cha
uzalishaji kuwa kikubwa sana.



“kwa sasa hasa ndani ya Mkoa wa Arusha Mjini unakuta kila mahali ni
benki lakini ukija vijijini hakuna hata benki ya kugeresha maisha sasa
hawa Wamiliki wa Mabenki  na Taasisi za Fedha wanasahau kuwa ambaye
anaweza kujikwamua zaidi kiuchumi ni mtu wa Kijijini kwa kuwa ndani ya
Vijiji kuna fursa Nyingi sana hasa za Kilimo, na Ufugaji hivyo basi
napenda kuwakumbusha kuwa mnatakiwa kuwakumbuka hata wananchi wa
Vijijini hata kwa kuwapa elimu ya kumiliki fedha”aliongeza Bw Kagenzi



Pia alisema kuwa mbali na Mabenki hayo kuweza kuwekeza zaidi Vijijini
lakini nao wafanyakazi hasa ambao ni waajiriwa wa Serikali wanatakiwa
kuijiendeleza kwa kuhakikisha kuwa wanatumia fursa mbalimbali za
Mabenki hasa NMB kwa kuhakikisha kuwa wanakopa na kisha kufanyia
Mikopo yao kazi za maendeleo kwa manufaa ya Jamii zao.



Awali Meneja wa Benki hiyo kwa kanda ya Kaskazini bi Vicky Bishubo
alisema lengo halisi la kuwakutanisha walimu wa shule mbalimbali ni
kuweza kuwapa elimu mbalimbali ikiwemo huduma zinazotolewa na Benki
hiyo hali ambayo itawafanya wadau hao kuweza kufikia malengo yao
mbalinbali ya Kimaisha.



“kama tunavyojua ni kuwa benki yetu mpaka sasa imeshatoa mikopo mingi
sana kwa walimu na walimu ni wadau wetu wa muhimu sana sasa
tunapowakutanisha hivi katika siku ya Mwalimu ndani ya benki hii
tunaweza kuwaongezea uwezo wa kutumia fursa zilizopo ambazo kama nazo
watazitumia vema basi wataweza kufikia malengo yao
mbalimbali’aliongeza Bi Vicky

Share this:

Post a Comment

unashauriwa kutoa maoni muda na wakati wowote na kama unahabari yeyote unaruhusiwa kututumia

 
Back To Top
Copyright © 2014 MOUNT KILI NEWS. Designed by OddThemes | Distributed By Gooyaabi Templates