BREAKING NEWS

Monday, November 12, 2012

TEJA ALIYEIBUKA KUWA MWANA SANAA AONGEA NA MO BLOG NA KUWAAMBIA VIJANA KUBWIA ‘UNGA’ NI KUCHUNGULIA KABURI


*MATEJA WAAMBIWA WACHAGUE MOJA KATI YA KIFO AU KUACHA MADAWA YA KULEVYA*
 MO BLOG: Tupe histioria fupi ya maisha yako..!
MWIRU: Naitwa Zakaria Antony Mwiru nikiwa mzaliwa wa Kusini mwa Tanzania lakini wazazi wangu walihamia Dar es Salaam nikiwa na umri wa miaka 2, hivyo nimekulia Dar es Salaam na kusoma Shule ya Msingi Kinondoni A na Nikasoma Shule ya Sekondari Kinondoni Muslim mpaka Kidato cha 4 bahati mbaya nilifeli hivyo nikajiunga na Chuo cha Sanaa Bagamoyo kwa muda wa miaka 3 nikasoma sanaa za ‘Wood Carvings’, ‘Sculpture’, ‘Painting’ na ‘Ngoma za Utamaduni’.
Baada ya kuhitimu kwa miaka mitatu nilifanya shughuli zangu za sanaa kwa muda wa kama miaka mitano hivi, na baadae nikajikuta nimeingia katika sakata la dawa za kulevya.
MO BLOG:  Badala ya kuendelea na sanaa uliyojifunza Bagamoyo ilikuaje ukaingia katika mkumbo wa matumizi ya dawa za kulevya.
MWIRU: Nahisi sababu iliyonipelekea kuingia kwenye mkumbo wa dawa za kulevya ni kutohisi kuwa na furaha kwa maisha ninayoishi na nikategemea kwamba nitapata furaha zaidi kama nitatumia ulevi, kwa hiyo nikaanza na bangi kisha pombe  na baadae nikaingia katika matumizi ya Heroin.
Lakini vile vile sikupata ile furaha niliyokuwa naitegemea na matokeo yakawa mabaya zaidi na baada ya muda mrefu nilichoshwa na ile hali iliyojaa mateso ndani yake.
MO BLOG: Umetumia dawa za kulevya kwa takriban miaka mingapi?
MWIRU: Nimetumia dawa za kulevya kwa takriban miaka 10, yaani ukichanganya tangu nianze kutumia pombe, bangi na unga, lakini hapo mwanzo nilitumia kama miaka minne kwenye bangi na pombe na miaka sita nikatumia na Heroin.
 MO BLOG: Unaweza ukatuelezea umepata madhara gani baada ya kutumia madawa hayo.?
MWIRU: Ndio; unajua kwenye hii program yetu tunasema ‘Siri Zetu Ndio Madhara Yetu’ sasa mimi dawa za kulevya zilinisababisha nikapata Hepatitis B. Hii ni homa ya ini lakini ambayo inaweza kutibika ambapo ningepata Hepatitis C ini lingekuwa limearibika kabisa. Niliambiwa kama ningeendelea kutumia ningepata Hepatitis C.  
Madhara mengine niliyopata japo sio makubwa sana nilipoteza uhusiano na ndugu zangu na familia yangu, nikapoteza uaminifu kwa watu wangu wa karibu vitu ambavyo viliniumiza sana.
MO BLOG: Uliijuaje na ilikuaje ukaingia ‘SOBER HOUSE’..?
MWIRU: Mara ya kwanza niliisikia ‘SOBER HOUSE’ lakini sikuweza kuingia. Lakini bahati nzuri nilikuwa na rafiki yangu alikuwa ni raia wa Sweden, alikuwa ananipenda na nilifanya nae biashara sana na kazi zangu alikuwa ana nunua mara kwa mara na alivutiwa nazo sana.
Siku moja aliniita akaniambia kuna swali anataka kuniuliza nika mwambia niulize tu! Akaniambia nimwambie ukweli kama natumia Heroine au situmii. Kwa hiyo mimi siku hiyo nikaona siwezi kufanya tena siri, kwa sababu siku zote alikuwa rafiki yangu lakini nilikuwa nimemficha.
Siku hiyo nikaamua nikakiri mbele yake kwamba natumia Heroin, baada ya kukiri akaniambia ananipenda sana na yuko tayari kunisaidia kuachana na matumizi ya Heroin. Akasema ni bora uvute bangi au unywe pombe kuliko kutumia Heroine. Akasema atanisaidia kuacha lakini itanikosti; nikakubali nikamwambia nitalipia hizo gharama.
Yeye ndiye aliyenipeleka ‘SOBER HOUSE’ akanilipia miezi mitatu akatoa kitu kama laki tano kwa ajili ya ada yangu na nyingine za matumizi yangu nitakapokuwa humu ndani. Hivyo sio uwezo wangu mimi lakini Mwenyezi Mungu alinichagua kwamba huyu mtu nataka nimuokoe lakini kupitia kwa mtu.
Na alikuwa ni mtu si wa kutoka kwenye familia yangu kwa sababu hata wazazi wangu nilikuwa naogopa hata kuwaambia natumia Heroin kwa sababu sikuona kama ni sifa nzuri. nisingeweza kwenda kuwaambia wanipeleke ‘SOBER HOUSE’ hivyo Mungu akanitumia mtu akanisaidia na mimi nikapokea ule msaada na mpaka sasa situmii tena madawa hayo. Na Yule m-Sweden aliniambia shukran nitakayompa ni kutotumia tena Heroine.
Msanii Zakaria Mwiru akionyesha sanamu ya Bi. Kidude kwenye maonyesho yaliyofanyika hivi karibuni.
MO BLOG: Yapi unaweza kuyataja kama mafanikio baada ya kuacha kutumia Heroin.?
MWIRU: Mafanikio ambayo naweza kuyataja baada ya kipindi hichi cha mwaka mmoja na miezi kadhaa tangu kuacha kutumia dawa, kwanza ninaweza nikafanya kazi bila kutumia kilevi, naweza kula chakula bila kutumia stimu na naweza kupata usingizi bila kutumia dawa kwangu ni mafanikio tosha, kwani mwanzo nilikuwa siwezi.
Kingine kwa sasa naweza kumiliki vitu vya material, kama simu, kompyuta, ipad na vingine kwa sababu zamani nilikuwa siwezi kuvimiliki nikivipata nawaza kuviuza ili nikapate dawa za kulevya.
MO BLOG: Vijana ambao bado mpaka sasa wanatumia madawa ya kulevya unawaambia nini.?
MWIRU:  Kwa sababu mimi mwenyewe nilitumia madawa ya kulevya kwa kipindi kirefu, nikajaribu kuacha nikashindwa na nilishindwa kwa sababu ya yale maumivu unayoyapata unapoacha, ningependa kuwaambia vijana wenzangu wavumilie hayo maumivi ya saa 72 tu kama siku tatu tu. Kama unavyojua ‘No Gain Without Pain’ kwa vijana nawaambia kuwa mwenyewe kuacha ni ngumu sana lakini tukiwa pamoja tukashirikiana inawezekana.
MO BLOG: Kuna kundi la vijana ambao hawajawahi kutumia dawa za kulevya , hawajui stimu yake, hawajui maumivu yake wala madhara yake, hawa unawaambia nini.?
MWIRU:  Vijana hawa nawahusia wasije wakasema najaribu nione raha yake itakaa vipi, kwa sababu hata mimi mwanzo nilijaribu nikaona kama nzuri mwisho wake ukawa mbaya. Nawahusia vijana wenzangu ambao hawajawahi kushika dawa wasianze; kwani wakigusa mara ya kwanza tu watakuwa wameingia kwenye maradhi ya uteja. Kikubwa wasiwe na tama ya kufanya mambo ya kuiga.
MO BLOG: Swali la kizushi vipi mahusiano yako na wanawake wakati unatumia dawa za kulevya.?
MWIRU: Kwanza nilikuwa na mahusiano mazuri na wanawake lakini nilipoanza kubwia mwanamke wangu alikuwa unga.
Kwa mfano mimi ni mwanasanaa hivyo katika biashara yangu walikuwa wakija wanawake kibao hasa wa kizungu wakifurahishwa na kazi zangu wengine walitaka mahusiano lakini sikuwa na dili nao nikuwa nawaza unga tu.
Nilikuwa nafanya nao biashara kwa ajili ya kupata hela, lakini niliwaambia sitaki kwenda Ulaya walanini.
Mimi ilikuwa badala nijenge daraja la kukutana na watu wazuri nilikuwa najenga ukuta naishi maisha ya kujitenga na kuishi maisha ya ubinafsi.
Pete aliyokabidhiwa na mama yake mzazi kama zawadi baada ya kuacha kutumia madawa ya kulevya.
MO BLOG: Baada ya kuacha kutumia dawa za kulevya mahusiano yako na familia yakoje?
MWIRU:  Uhusiano wangu na familia mpaka sasa hivi naweza kusema umekaa vizuri, kwa sababu baada ya kuacha dawa hizi nilikwenda kwa mama yangu na akanikumbatia kwa mara ya kwanza ikiwa imepita zaidi ya miaka 10 hajawahi kunikumbatia. Na akanionyesha upendo na kunizawadia pete akaniambia hii pete yako ya Baraka. Akaniambia kuwa na kama utataka tena kuvuta madawa hii pete yangu nirejeshee.
MO BLOG: Kwa kifupi tuambie kuhusu haya maonyesho ya SOBER HOUSE na utaratibu mzima na pengine mtu anataka kujiunga lakini hana uwezo.?
MWIRU: Kuna utaratibu mzuri umeandaliwa kwa sababu mtu anapotaka kujiunga sio lazima alipe kwa mkupuo, anaweza akalipa awamu ya kwanza kwa malipo ya dawa zake za maumivu anapokuwa ndani ya nyumba halafu, nyingine ni kwa ajili ya matumizi yake kama maji, kulala, umeme n.k.
Na wakati huohuo anashiriki masomo.
MO BLOG: Je waonaje hicho kiwango mnacholipia, mtu wa kawaida anayetumia dawa za kulevya kama mpiga debe anaweza kukimudu?
MWIRU: Kwa kweli kama ndio umeshaanza kutumia na kufukuzwa nyumbani kiwango hicho ni kikubwa, lakini mtu huyu anahitaji msaada kwa wasamaria wema kwa sababu ukiangalia tu kula yake kwa siku inazidi 3000. Naweza kusema.
MO BLOG: Kwa uzoefu wako unadhani nini hasa kinacho wapelekea vijana kukimbilia kwenye utumiaji wa madawa ya kulevya.
MWIRU: Vijana wanakimbilia kwenye matumizi ya dawa za kulevya kwanza hawajui tatizo lake ni nini? Nadhani wengi wanakosa furaha na kudhani furaha wataipata kwenye matumizi hayo; cha msingi elimu inapaswa kuenezwa kwa vijana sio tu kukabili dawa za kulevya ila pia kubadili mwenendo mzima wa maisha haswa kufundishwa ustahimili.
MO BLOG: Kwa kumalizia Bw. Mwiru nini ushauri wako kwa watanzania kwa ujumla, kwa maana ya serikali, taasisi, wizara, vijana watumiaji na wasiotumia.
MWIRU: Kwanza kwa vijana wanaotumia wajaribu kutafuta wadhamini au wakiweza warudi kwa familia zao waombe kusaidiwa kwa sababu peko huwezi. Na kujikubali kwamba wana matatizo ya kutumia dawa.
Naiomba jamii isiwanyanyapae watu wanaotumia dawa za kulevya na kuwaona kama hawafai bali ichukulie kuwa ni njia moja mtu ameteleza na mtu huyo huyo kama atanyanyuliwa akatembea tena kwa miguu yake.
Kwa serikali natoa wito kutoa misaada katika hizi nyumba za kusaidia watu walioathirika na dawa za kulevya kama ilivyo ‘SOBER HOUSE’ ili ziweze kuwaelimisha vijana kutotumia dawa za kulevya.
Kwa sababu hatutaweza kuzuia watu wasiingize dawa za kulevya kwa sababu hata mataifa makubwa duniani yameshindwa kuzuia kwa hivyo msingi ni kuwaelimisha kutotumia, naamini watu wetu wakielimika soko la dawa hizo litazidi kupungua.
MO BLOG:  Nini kilikupelekea mpaka ukachonga sanamu ya Bi. Kidude? Na sio mtu mwingine maarufu Tanzania.
MWIRU: Ahh unajua nilipoingia Zanzibar mara ya kwanza nilimsikia Bi. Kidude kupitia filamu moja inaitwa maangamizi. Ilikuwa inazungumzia watu waliokuwa wanadharau wahenga na mambo ya kale. Nilivutiwa nayo sana kwa sababu huyu bibi nilimuona ni mwanamke anayeweza kusimamia utamaduni wa kiafrika.
Bi. Kidude namfananisha kama balozi wa Zanzibar anayewakilisha utamaduni wa Zanzibar kimataifa.Ndio maana nikavutiwa kutengeneza sanamu yake kwa sababu ameweza kustiki katika performing act tangu awali na mpaka sasa.
MO BLOG: Nani mwingine maarufu unafikiria kuchonga sanamu yake.?
MWIRU:  Baada ya hapa nafikiria kuchonga sanamu ya sura ya kila kiongozi aliyepita katika nchi hii.
MO BLOG: Haya ndugu yetu hapa Kassim Rashid jitambulishe wa wadau wa Mo Blog.
Baada ya kufahamu mengi kuhusu Zakaria Mwiru Mo Blog ilizungumza na meneja wa Sober House.
RASHID KASSIM:  Mimi ndie meneja wa nyumba inayoshughulika na kufanya ‘exhibition’ hii. Hii nyumba inaitwa ‘Sober House’ ambayo ipo maeneo ya Mpendae Zanzibar.
MO BLOG: Vikwazo gani unakabiliana navyo kuendesha nyumba hii ukizingatia unadili na watu waliokuwa tayari wamepinda kwa madawa?
RASHID KASSIM:  Vikwazo ni vingi kwa kweli ikiwemo malipo ya hawa watu wanaoletwa ndani ya nyumba. Kwa sababu sio muda wote wanafanya malipo kwa wakati muafaka nah ii inatupa ugumu sana inabidi watu kutoa fedha mifukoni mwao kwa ajili ya kuendesha nyumba hii.
Kikwazo kingine ni kama unavyojua watu waliomo humu ni wenye tabia tofauti hivyo inabidi kuwa na ustahimilivu na busara ili kuweza ku-‘deal’ nao.
MO BLOG: Wewe mwenyewe umewahi kutumia kama ndi kwa muda gani na ilikuaje ukaacha.
RASHID KASSIM: Ndio mimi nimetumia si chini ya miaka 15. Ilifika kipindi nikawa na machaguo mawili tu ama nife au niache tumia madawa. Kwa katika machagua hayo lililokuwa bora kwa niliona bora niache kuliko kufa. Kwa sasababu hata ningekufa bado tatizo lilikuwa nakufa katika kifo cha aina gani.
MO BLOG: Kwa ufupi tuelezee mafanikio baada ya kuanzisha nyumba hii.
RASHID KASSIM: Kwa kweli mafanikio ni mengi sana maana nyumba yetu hii ndio imezaa nyumba nyingine hizi zilizopo sasa za kuwasaidiwa watu wanaotumia dawa za kulevya.
Kingine ni kwamba tumepiga hatua kutoka katika ‘Recover’ tumekuja katika Sanaa. Japo mimi mwenyewe sifanya sanaa ila ndio msimamizi wa hawa wenzangu.
MO BLOG: Tunawashukuru sana Meneja Rashid Kassim Na Msanii Zakaria Mwiru kwa jitihada zenu katika kupambana na wimbi la matumizi ya dawa za kulevya na pia kuendeleza sanaa hapa nchini.
RASHID KASSIM NA ZAKARIA MWIRU: Akhsanteni sana Bwana Lemmy na Zainul tunaomba muendelee kutungaza hivi na blogs nyingine ziige mfano wenu ili vijana ambao bado wanatumia wajue bado wana nafasi ya kuacha na kujiendeleza.


Share this:

Post a Comment

unashauriwa kutoa maoni muda na wakati wowote na kama unahabari yeyote unaruhusiwa kututumia

 
Back To Top
Copyright © 2014 MOUNT KILI NEWS. Designed by OddThemes | Distributed By Gooyaabi Templates