Mwendesha Mashitaka wa
Mahakama ya Kimataifa ya Makosa ya Jinai (ICC) wiki hii imetoa wito wa
ushirikiano zaidi baina ya nchi katika kushughulikia uhalifu uliofanywa
nchini Libya, wakati mahakama moja nchini Sweden imemshitaki raia wake
mmoja mwenye asili ya Rwanda kwa mashitaka ya mauaji ya kimbari.
SWEDEN
Mahakama yamshitaki raia wa Sweden mwenye asili ya Rwanda: Mahakama
moja nchini Sweden Jumatatu ilimshitaki raia wake mmoja mwenye asili ya
Rwanda kwa madai ya kushiriki katika mauaji ya kimbari ya mwaka 1994.
Mwendesha mashitaka alisema kesi yake imepangwa kuanza kusikilizwa
kuanzia Ijumaa ijayo na itakuwa kesi ya kwanza ya aina hiyo kuwahi
kusikilizwa nchini Sweden.Mtu huyo anadaiwa kutenda uhalifu huo mkoani
Kibuye, Magharibi ya Rwanda.
RWANDA
Ngoga aishutumu Uingereza jinsi inavyoshughulikia watuhumiwa wa
mauaji ya kimbari: Mwendesha Mashitaka Mkuu wa Rwanda, Martin Ngoga,
Jumatatu iliishutumu Uingereza kwa kutoshughulikia ipasavyo kesi za
watuhumiwa wa mauaji ya kimbari waliomo nchini humo.Alikuwa anajibu
ripoti moja iliyoandikwa na vyombo vya habari nchini Uingereza kwamba
mnyarwanda mmoja, Modeste Kennedy, anayedaiwa kushiriki katika mauaji ya
kimbari ya mwaka 1994, yuko nchini humo akifanya kazi kama dereva wa
taksi na kwamba hawezi kurejeshwa nchini Rwanda kukabiliana na mashitaka
dhidi yake kutokana na uzingatiaji wa haki za binadamu.
ICTR
ICTR yapania kuhitimisha kesi zake ifikapo 2014: Maafisa wa Mahakama
ya Kimataiafa ya Mauaji ya Kimbari ya Rwanda (ICTR) Alhamisi walitangaza
kwamba mahakama hiyo itahitimisha kesi zake zote ifikapo mwishoni mwa
mwaka 2014 kulingana na muda uliopangwa. Maafisa hao wamesema hivi sasa
mahakama hiyo ina majukumu mawili muhimu.La kwanza, kuhitimisha
usikikilza wa hatua ya awali ya kesi ya mwisho na pia kukamilisha hukumu
za kesi katika ngazi ya rufaa na maamuzi mbalimbali yaliyosalia.
ICC
Mwendesha mashitaka wa ICC ahimiza ushirikiano: Mwendesha Mashitaka
wa ICC, Fatou Bensouda Jumatano ilitoa wito wa kushirikiana zaidi baina
ya nchi na mashirika mbalimbali ya Umoja wa Mataifa katika kushughulikia
uhalifu uliofanywa nchini Libya. Bensouda alikuwa anawasilisha ripoti
ya nne juu ya hali ya Libya, mbele ya Baraza la Usalama la Umoja wa
Mataifa. Alisema tangu Machi 2011 mahakama hiyo ilipofungua upelelezi
juu ya uhalifu wa kimataiafa uliotendeka katika nchi hiyo ya Afrika
Kaskazini, imekwisha toa maombi ya kutaka usaidizi 130 na mengi kati ya
hayo hayajatekelezwa.
Post a Comment
unashauriwa kutoa maoni muda na wakati wowote na kama unahabari yeyote unaruhusiwa kututumia