BREAKING NEWS

Wednesday, November 7, 2012

RAIS WA JAMUHURI YA MUUNGANO WA TANZANIA AKAGUA MIRADI 19 KWA MUDA WA WIKI MOJA


TAARIFA KWA VYOMBO VYA HABARI

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Jakaya Mrisho Kikwete amerejea Dar es Salaam mchana wa leo, Jumanne, baada ya kumaliza ziara ya siku tisa katika mikoa minne ambako amekagua, kuanzisha ama kuzindua miradi 19 ya maendeleo na kutembea kiasi cha kilomita 2,770.
Rais Kikwete amewasili Dar es Salaam akitokea Dodoma ambako amefanya ziara ya kikazi ya siku mbili baada ya kumaliza ziara katika mikoa ya Kilimanjaro, Arusha, Manyara na Singida.
          Katika Mkoa wa Kilimanjaro ambako Rais Kikwete alianzia ziara yake Oktoba 28, mwaka huu, miongoni mwa mambo mengine alikagua nyumba za wahanga wa maporomoko ya mwaka 2006 kwenye kijiji cha Goha na akafungua Kiwanda cha Kusindika Tangawizi kilichoko Mamba Miamba, Wilaya ya Same, na akafungua Shule ya Sekondari ya Kata ya Asha Rose Mingiro iliyoko mjini Mwanga.
Miradi mingine aliyoifungua Rais Kikwete katika Mkoa wa Kilimanjaro ni uzinduzi wa barabara za Rombo Mkuu-Tarakea na Kwasadallah-Masama na akafungua Ofisi ya Mkaguzi Mkuu na Mdhibiti wa Hesabu za Serikali (NAO) mjini Moshi.
Katika Mkoa wa Arusha, Rais Kikwete alizindua Hospitali ya Wilaya ya Arusha ya Olturumet, akazindua Mradi Mkubwa wa Uboreshaji wa Miji kwa kufungua barabara za Jiji la Arusha, akazindua Jiji la Arusha, akafungua rasmi Chuo Kikuu cha Sayansi na Teknolojia cha Nelson Mandela na akatembelea Kiwanda cha Nguo cha A-Z.
Kabla ya kuondoka Mkoani Arusha, Rais Kikwete alifungua Shule ya Msingi ya Sokoine na kuzindua ukarabati mkubwa wa Barabara ya Minjingu-Arusha.
Mkoani Manyara, Rais Kikwete alifungua rasmi Barabara ya Singida-Minjingu-Arusha, akazindua mradi mkubwa wa maji wa Mji wa Babati na akaweka jiwe la msingi kwenye ujenzi wa Barabara ya Babati-Bonga.
Mkoani Singida, Rais Kikwete alizindua mradi mkubwa wa maji wa Mwankoko kwa ajili ya Mji wa Singida, akaweka jiwe la msingi kwenye ujenzi wa Barabara ya Manyoni-itigi-Chaya na akafungua Barabara ya Issuna-Manyoni.

Imetolewa na:
Kurugenzi ya Mawasiliano ya Rais,
Ikulu.
Dar es Salaam.
6 Novemba, 2012

Share this:

Post a Comment

unashauriwa kutoa maoni muda na wakati wowote na kama unahabari yeyote unaruhusiwa kututumia

 
Back To Top
Copyright © 2014 MOUNT KILI NEWS. Designed by OddThemes | Distributed By Gooyaabi Templates