BARAZA LA MADIWANI LONGIDO LAKATAA MWEKEZAJI WA MAGADI KUJENGA KIWANDA HICHO MONDULI

Baraza la Madiwani wa Halmashauri ya Longido limesema kuwa halitakubaliana na mwekezaji wa kujenga kiwanda cha Magadi kujengwa katika wilaya ya Monduli na Malighafi hiyo kuchukuliwa katika wilaya ya Longido.

Akizungumza katika baraza la madiwani lililofanyika katika wilaya hiyo makamu mwenyekiti wa halmashauri hiyo Esupat Ngulupa alisema kuwa haiwezekani mali ghafi zote zipatikane katika wilaya ya longido alafu mwekezaji akajenge kiwanda katika wilaya nyingine.

Esupat alisema kuwa ni lazima madiwani waoneshe msimamo katika kujali maslahi ya wananchi wa longido  kwa umuhimu mkubwa sana kwa kuwa mchakato huo tangu mwanzo ulikuwa unaonesha kuwa kiwanda cha uvunaji wa magadi yaani (SODA ASH MINING) kitajengwa katika wilaya  tayarimadiwani walishaanza mchakato wa kufuatilia kwa karibu mpango huo ikiwa ni pamoja na kufanya ziara nchini Kenya.

“Nataka  niwahakikishie kuwa hatutakubali kiwanda kijengwe Wilaya ya Monduli wakati magadi hayo yanapatikana ziwa natron ambalo lipo hapa kwetu hatutakubali mana tunajua wazi kuwa mwekezaji atakuwa amepewa taarifa tofauti kwa hili hatutakubali kabisa longido inajitegemea na monduli vivyo hivyo.”alisema Esupat

Aliongeza kuwa Rasilimali hiyo ni muhimu sana hivyo ni lazima kiwanda hicho kijengwe wilayani longido ili kiwanufaishe wakazi wa eneo hilo kutokana na vitendea kazi ambavyo vinapatikana wilayani hapo.

Kwa upande wake mwenyekiti wa halmashauri hiyo Joseph Ole Sadira alisema kuwa madiwani wa halmashauri hiyo wanaunga mkono kwa asilimia mia moja mwekezaji huyo kujenga kiwanda hicho katika wilaya ya longido ili kiweze kuwanufaisha wananchi wa eneo hilo.

Pia alisema kuwa tayari madiwani walishafanya ziara nchini Kenya ili kujionea jinsi wanavyofanya kazi hiyo na mafanikio ambayo wameyapata  kutokana na uvunaji wa magadi hiyo na amebainisha kuwa magadi yaliyopo wilayani hapo ni bora kuliko yanayopatikana Kenya.

Sadira alisema kuwa tayari Wilaya hiyo ilishaufuatilia uwekezaji huo kwa kina na zaidi na kuingia hata nchi jirani na kuchunguza faida za uvunaji huo katika kiwanda kilichopo nchini Kenya

Alisema kuwa kutokana na utafiti uliofanywa ulibainsha faida kubwa sana itapatikana kama watajiingiza katika mradi huo hivyo hawatakubaliana na mwekezaji kuchukua malighafi hiyo na kunufaisha wananchi wa wilaya nyingine ili hali waliopo hapo hawanufaiki na chochote.

Naye mkurugenzi  mtendaji Julius Chalya alikiri kuwa tayarimadiwani walishafanya ziara katika nchi jirani kama Kenya na kujionea mafanikio waliyoyapa kutokana na uwekezaji huo hivyo kuwepo kwa kiwanda hicho katika wilaya ya longido kutaleta tija sana  na maendeleo kwa wilaya hiyo ambayo kwa kiasi kikubwa wananchi wake ni jamii ya Wafugaji.


Post a Comment

unashauriwa kutoa maoni muda na wakati wowote na kama unahabari yeyote unaruhusiwa kututumia

Previous Post Next Post