KINANA KUPOKELEWA KESHO ARUSHA KWA MBWEMBWE

CHAMA cha mapinduzi(CCM) mkoani Arusha kinataraji kumpokea  na kumkaribisha nyumbani katibu mkuu mteule wa CCM taifa,Abdulraham Kinana leo katika uwanja mdogo wa ndege uliopo Kisongo nje kidogo ya jiji la Arusha ambapo pia atapata fursa ya kuwahutubia wafuasi wa chama hicho mkoani hapa sanjari na kufungua mashina mbalimbali ya wakereketwa.

Katika mapokezi hayo Kinana ataambatana na katibu wa itikadi na uenezi,Nape Nnauye,naibu katibu mkuu wa CCM bara,Mwigulu Nchemba pamoja na wajumbe mbalimbali wa sekretarieti Mmpya ya CCM ambapo  wanataraji kuongoza mashambulizi ya kushambulia ngome ya Chadema ambayo inasemekana kujikita mkoani hapa.
 
Akiongea na waandishi wa habari juzi jijini hapa,katibu wa siasa na uenezi wa CCM mkoani hapa,Isaac Kadogoo alisema kwamba mkutano huo utafanyika novemba 24 mwaka huu ambapo kutakuwa na maandamano makubwa ya kumpokea Kinana kuanzia uwanja mdogo wa ndege uliopo Kisongo jijini hapa hadi wilayani Arumeru na kisha kurejea katikati ya jiji la Arusha.
 
Kadogoo,alisema kwamba lengo la shughuli hiyo ni kumkaribisha Kinana ambaye ni mkazi wa mkoani Arusha sanjari na kuelezea sera mbalimbali yakiwemo maendeleo yaliyoletwa na CCM mkoani Arusha na nchini kwa ujumla.
 
Hatahivyo,katibu huyo wa siasa na uenezi alisema kuwa viongozi mbalimbali wa CCM taifa watapata fursa ya kuwahutubia wakereketwa wa chama hicho katika uwanja wa Sheikh Amri Abeid sanjari na wakazi wa Arusha katika mkutano ikiwa ni pamoja na  kuongoza  uzinduzi wa matawi hayo.
 
Alisisitiza kwamba hadi sasa taratibu mbalimbali za maandalizi kwa ajili ya shughuli hizo yamekamilika kwa asilimia mia moja ambapo katika maandamano ya kumpokea Kinana kutakuwa na msafara  wa magari,pikipiki pamoja na watembea kwa miguu.
 
Hatahivyo,aliwataka wanachama wa CCM mkoani Arusha kujitokeza kwa wingi katika sherehe hizo huku akienda mbali na kudai kuwa kutakuwa na vikundi mbalimbali vya ngoma na wasanii watakaotumbuiza kusindikiza sherehe hizo.
 
Katika hatua nyingine,Kadogoo alijitapa kwamba Chama hicho kimejipanga kikamilifu kushinda katika uchaguzi mdogo wa ubunge katika jimbo la Arusha mjini endapo mahakama kuu ya rufaa nchini ikitupilia rufaa iliyowasilishwa na mbunge wa zamani wa jimbio hilo,Godbless Lema.
 
“Naomba nieleweke kwamba CCM tumejipanga na kujidhatiti kushinda uchaguzi mdogo wa ubunge katika jimbo la Arusha mjini endapo rufaa ya Lema ikitupiliwa mbali na mahakama kuu ya rufaa na ujio wa Kinana tunaamini utatikisa hapa mjini”alijitapa Kadogoo
 

Post a Comment

unashauriwa kutoa maoni muda na wakati wowote na kama unahabari yeyote unaruhusiwa kututumia

Previous Post Next Post