MAMLAKA ya mapato(TRA) mkoani Arusha imejitolea misaada
mbalimbali yenye thamani ya zaidi ya sh,6 milioni kwa vituo mbalimbali vya
yatima vilivyopo jijini Arusha kama hatua ya kusheherekea siku la mlipa kodi
nchini inayotimiza kilele chake leo.
Misaada hiyo iliyoendana na fedha taslimu ilikabidhiwa na
kaimu meneja wa mamlaka hiyo mkoani Arusha,Theresia Mponeja katika vituo vya The
Chiristian Women ,Faraja Orphan sanjari
na kituo cha Kibowa Orphanage kilichopo Lemara jijini hapa.
Akikabidhi misaada hiyo juzi,Mponeja alisema kwamba lengo la
kutoa misaada hiyo ni baada ya mamlaka yao kuguswa na tatizo la watoto yatima
hapa nchini hususani katika kipindi hiki cha maadhimisho ya siku ya mlipa kodi.
Alisema kwamba wao wamekuwa wakikusanya kodi mbalimbali hapa
nchini na hivyo wameamua kurudisha faida yao mbele ya jamii hiyo ikiwa ni
pamoja na kusaidia watoto yatima.
Mponeja aliitaja misaada mbalimbali waliyoitoa kuwa ni
pamoja na sukari,vyandarua,mashuka,vifaa vya
mashuleni,mchele,sabuni,unga,viatu,nguo za watoto pamoja na magodoro kwa ajili
ya vituo hivyo.
Naye mkuu wa kituo cha The Christian Women,Zakia Khatibu pamoja na katibu wa kituo cha Faraja,Faraja Ngugi
waliushukuru uongozi wa mamlaka hiyo kwa kuwajali kwa kuwakumbuka huku
wakiwataka wahisani mbalimbali kuiga mfano huo.
Naye,mtoto Bahati Sungura anayelelewa katika kituo cha
Faraja Orphan ambaye anasoma katika shule ya sekondari ya Kimandolu aliishukuru
mamlaka hiyo kwa kumsaidia ada ya shule kiasi cha sh,300,000 huku akidai kwamba
alikaa ndani ya kituo hicho kwa muda wa wiki mbili na kushindwa kuhudhuria
masomo kwa kukosa ada.
Akipokea ada hiyo,katibu wa kituo hicho,Faraja aliuambia
uongozi wa mamlaka hiyo kwamba ni jambo jema kumkwamua mwanafunzi huyo na
kusisitiza kwamba ataziwasilisha fedha hizo mbele ya uongozi wa shule na kisha
kuwapatia risiti ya malipo kama ushahidi mzuri.
Post a Comment
unashauriwa kutoa maoni muda na wakati wowote na kama unahabari yeyote unaruhusiwa kututumia