Mkuu wa Wilaya ya Simanjiro Mkoani
Manyara,Brigedia Jenerali Cosmas Kayombo ameuagiza uongozi wa wilaya hiyo kutoa
tuzo kwa watu wanaopanda miti ili kutunza mazingira na kukabiliana na
mabadiliko ya tabia nchi.
Brigedia Jenerali Kayombo aliyasema hayo juzi
mji mdogo wa Mirerani kwenye mdahalo wa mabadiliko ya tabia nchi na namna ya
kupunguza athari zake uliondaliwa na mtandao wa asasi za kijamii mkoani humo
Macsnet
na The Foundation for Civil Society.
Alisema ili
kuhakikisha jamii inapenda kutunza mazingira kwa kupanda miti uongozi wa wilaya
hiyo unatakiwa kujipanga kutoa tuzo kwa washindi wa upandaji miti ili kuongeza
hamasa ya kutunza mazingira wilayani humo.
Alisema mabadiliko
ya tabia nchi ni suala ambalo hivi sasa linazungumzwa na
wasomi,wanasayansi,wanasiasa na jamii kwa ujumla hivyo juhudi zinapaswa
kufanyika ili kuhakikisha mabadiliko ya tabia nchi yanadhibitiwa.
“Juhudi za
makusudi,elimu na sera ziendelee kutolewa kwa jamii kwani uelewa mdogo na
dhamira ya wenye dhamana ni ya mashaka katika kukabiliana na mabadiliko ya
tabia nchi hivi sasa,” alisema Brigedia Jenerali Kayombo.
Mtoa
mada Jackson Muro alisema madhara ya mabadiliko ya tabia nchi ni ukame,magonjwa
ya binadamu,mifugo,wanyama na mimea,mafuriko yasiyotegemewa,sunami theluji kuyeyuka,kukosekana mvua na kina cha
bahari au ziwa kupungua.
Alisema
namna ya kupambana na mabadiliko ya tabia nchi ni kutunza uoto wa
asili,kupunguza uzalishaji wa hewa na gesi,kupanda miti ili inyonye hewa ukaa
inayopanda angani na kuchanganya mazao ya kawaida na misitu.
“Kwa
mujibu wa utafiti uliofanywa na shirika la chakula duniani FAO mwaka 2005
ulionyesha kiwango cha ukataji misitu duniani umefikia hekta milioni 7.3
milioni kwa mwaka hivyo hewa ya ukaa kushindwa kufyozwa,” alisema Muro.
Naye,mmoja kati ya washiriki wa mdahalo
huo,Kaanael Minja alimuuliza mkuu huyo wa wilaya nani anatoa kibali cha kukatwa
mkaa wilayani humo kwani hivi sasa uuzwaji wa mkaa umeenea na hakuna hatua
inayochukuliwa.
Hata hivyo,Brigedia Jenerali Kayombo alisema
hakuna kibali kinachotolewa na mtu cha kukata mkaa kwenye wilaya hiyo,hivyo
ushirikiano baina ya viongozi na jamii uongezwe ili kukomesha hali hiyo kwani
kijiografia Simanjiro ni kubwa.
Post a Comment
unashauriwa kutoa maoni muda na wakati wowote na kama unahabari yeyote unaruhusiwa kututumia