BARAZA la Madiwani wa Halmashauri ya Wilaya ya Simanjiro Mkoani Manyara limetoa maamuzi magumu kwa kuwaondoa kwenye nafasi zao wakuu wanne wa idara tofauti za wilaya hiyo kwa kukiuka miiko ya kazi zao.

Walioondolewa kwenye nafasi hizo ni Ofisa Elimu msingi wa wilaya hiyo Jackson Mbise,Ofisa Kilimo,Mifugo,Ushirika na Uvuvi Hamad Lyimo,Ofisa Wanyamapori Titus Towo na Ofisa Misitu na Nyuki Khalifan Nyala.

Mwenyekiti wa Kamati ya Elimu,Afya na Maji,Sumleck Ole Sendeka alisema Ofisa Elimu msingi,Mbise aliwashusha cheo bila kuwaondoa kwenye vituo waratibu elimu na walimu wakuu ambao wanafunzi wao walifaulu bila kujua kusoma na kuandika.

“Hali hiyo ilileta mtafaruku wilayani kwetu kwani hakushirikisha mtu hivyo waratibu na walimu wakuu 15 warejeshwe kwenye nafasi zao na wachukuliwe hatua stahiki na mamlaka ya nidhamu kwani hawakutendewa haki,” alisema Sumleck.

Mwenyekiti wa Kamati ya Uchumi,Ujenzi na Mazingira,Charles Kagaruki alisema Lyimo anaondolewa kwenye nafasi hiyo kwa vile hakuwasilisha makabrasha kwa wajumbe wa kamati hiyo kwa wakati husika hivyo amelewa madaraka.

Makamu Mwenyekiti wa halmashauri hiyo,Jackson Sipitek alisema Towo na Nyala wanaondolewa kwenye nafasi zao kutoka na kushindwa kudhibiti vitendo vya ujangili na uwindaji haramu ambao umekithiri hivi sasa wilayani humo.

Diwani wa kata ya Endiamtu Lucas Zacharia alisema baadhi ya watumishi wa idara ya misitu wanafanya kazi kwa mazoea kwani juzi alikamata gari lenye magunia 120 ya mkaa na alipowapigia simu walimuuliza gari hilo ni la nani.

“Urasimu wa kitengo hicho utaturudisha nyuma yaani mpaka ujuwe gari ni la nani ndiyo uje,madiwani walipitisha sheria ya kutaifisha mkaa na gari lilipe sh1 milioni ili uchomaji mkaa usiendelee hapa Simanjiro,” alisema Zacharia.

Hata hivyo,Mwenyekiti wa Halmashauri ya wilaya hiyo,Peter Tendee alisema Baraza hilo halina chuki binafsi na watumishi hao walioondolewa nyadhifa zao ila wanachoangalia ni maslahi ya wananchi wa Simanjiro.

“Kila mmoja anapaswa kutekeleza majukumu yake katika kuhakikisha kuwa utekelezaji na ufanisi unakidhi haja ya watu wa wilaya ya Simanjiro na hatupo hapa kwa ajili ya kumuonea mtu ila tunaangalia utendaji kazi,” alisema Tendee.