KESI ya
madai inayomkabili mfanyabiashara ambaye
pia ni mmiliki wa hoteli ya Snowcrest jijini Arusha,Wilfred Tarimo imehairishwa
tena juzi katika mahakama ya biashara kanda ya Arusha hadi desemba 14 mwaka huu
mara baada ya upande wa mdaiwa kukataa
kulipa kiasi cha fedha na riba anachodaiwa katika kesi hiyo.
Kesi
hiyo nambari 9 ya mwaka 2012 mkurugenzi wa kampuni ya Grand Alliance
Limited,James Ndika amefungua madai dhidi ya mmiliki wa hoteli ya Snowcrest
Hotel and Wildlife Safaris Ltd ambaye ni
Tarimo ambapo katika shauri hilo mdai analalamika kutapeliwa jumla ya kiasi cha
$ 1.7 milioni sawa na sh,3 bilioni kwa ajili ya mauziano ya hoteli hiyo.
Katika kesi
hiyo mlalamikaji anadai kwamba mmiliki
huyo wa Snowcrest alimuuzia hoteli hiyo mnamo novemba mwaka 2011 na kumpatia hati mbili za eneo la hoteli
hiyo lakini baadaye ilikuja kugundulika kwamba eneo la hoteli hiyo lina hati
tatu .
Katika kesi
hiyo mlalamikaji amedai kwamba hati moja kati ya hizo tatu ina mkopo wa kiasi
cha sh,1.5 bilioni kupitia benki mojawapo hapa nchini ambapo mara baada ya kubainika
ilikwamisha biashara ya mauziano ya hoteli hiyo.
Katika
shauri hilo Ndika anaomba alipwe kiasi chote cha fedha alizotoa kwa ajili ya kuinunua
hoteli hiyo sanjari na riba tangu siku ya mauziano kwa kuwa mmiliki wa
hoteli hiyo alimdanganya na kumpatia hati mbili lakini kumbe badala yake ina hati tatu.
Mbele ya
jaji anayesikiliza shauri hilo, Nyangarika alisema kwamba mara baada ya hatua
ya usuluhishi kukwama katika kesi hiyo kufuatia upande wa mdaiwa kukataa kulipa
kiasi hicho cha fedha na riba kwa mamlaka aliyonayo ameamua kuiharisha kesi hiyo hadi desemba 14
mwaka huu hadi pale mahakama itakapopanga tarehe ya kuanza kuisikiliza .
Mara baada
ya jaji Nyangarika kutoa kauli hiyo aliwauliza mawakili wa pande zote mbili
endapo wamekubalina na uamuzi wake na ndipo walipotamka kwa nyakati tofauti
kwamba hawana pingamizi juu ya kauli
hiyo na kisha kesi hiyo kuharishwa .
Katika kesi
hiyo upande wa mlalamikaji unawakilishwa na wakili Melkizedeck Lutema huku
upande wa mlalamikiwa unawakilishwa na wakili,Nelson Merinyo.