CHUO cha Ualimu Monduli mkoani Arusha, kimeazimia kuboresha michezo
shuleni kwa kuzalisha walimu waliofundishwa mbinu mbalimbali za kuibua
na kukuza vipaji kwa wanafunzi.
Walimu hao watakuwa wakifundisha michezo kama masomo ya kawaida,
badala ya mfumo wa sasa wa michezo kuwa kama vipindi vya ziada baada ya
masomo.
Akizungumza kwenye uwanja wa michezo wa
kumbukumbu ya Sheikh Amri Abeid hivi karibuni, mkufunzi wa michezo
chuoni hapo, Lamon Mtweve, alisema katika kutekeleza hilo, uongozi
umeendesha kozi maalumu kwa walimu wenye mwamko wa michezo, ili
wakatumike katika shule watakazokwenda kufundisha kwa ajili ya
kusimamia michezo na kukuza sekta hiyo ambayo imekuwa ikifanya vibaya
katika siku za hivi karibuni.
“Hii kozi tunayofundisha si tu kwa ajili ya kwenda kuwafundisha
wanafunzi masuala ya michezo mashuleni, bali pia itawasaidia walimu
watakaowakuta huko kufaidika, hasa wale waliosoma nje ya chuo chetu
ambao hawajasoma michezo wala hawaijui,” alisema.
Aliongeza kuwa kwa upande wa wanafunzi watajifunza michezo ya aina
mbalimbali, badala ya kushiriki ile iliyozoeleka kama soka na netiboli,
kwani walimu hao wanaandaliwa kuwa wataalamu wa michezo ya aina
mbalimbali kama riadha, tenisi, wavu, mikono, kuogelea, n.k.