UTANGULIZI:
Wizara ya Afya na Ustawi wa Jamii inapenda kutoa taarifa kwa umma juu
ya kuwepo kwa ugonjwa wa homa ya dengue yaani “dengue fever” hapa
nchini. Ugonjwa huu umethibitishwa baada ya sampuli zilizochukuliwa
kutoka kwa watu waliohisiwa kuwa na ugonjwa huu jijini Dar es salaam kupelekwa
kwenye maabara yetu iliyopo katika Taasisi ya Taifa ya Utafiti wa Magonjwa ya
Binadamu, Dar es salaam na kuthibitisha kuwa na virusi vya homa ya dengue mnamo
tarehe Juni 12, 2013. Utafiti huu uliongozwa na jopo la wataalamu kutoka Wizara
ya Afya na Ustawi wa Jamii ikishirikisha program ya mafunzo ya Epidemiolojia
yaani “Field Epidemiology and Laboratory Training Program” pamoja na
manispaa ya Ilala.
Hadi sasa idadi ya wagonjwa ambao waliogundulika kuwa na dalili za ugonjwa
huu ni 20 na hakuna mgonjwa yeyote aliyepoteza maisha.
HOMA YA DENGUE:
Homa ya dengue ni ugonjwa unaosababishwa na kirusi ambacho kinaenezwa na
mbu wa aina ya Aedes.
Dalili za ugonjwa huu ni homa, kuumwa kichwa, maumivu ya viungo
na uchovu Dalili hizi huanza kujitokeza kuanzia kati siku ya 3 na 14
tangu mtu alipoambukizwa kirusi cha homa ya dengue. Kwa wakati
mwingine dalili za ugonjwa huu zinaweza kufanana sana na dalili za
malaria, hivyo basi wananchi wanaombwa kuwa wakati wakipata homa kuhakikisha
wanapima ili kugundua kama wana vimelea vya malaria ua la ili hatua stahiki
zichukuliwe.
Virusi vya homa ya dengue vinaenezwa kwa
binadamu baada ya kuumwa na mbu aina ya “Aedes”. Mbu
hawa hupendelea kuzaliana kwenye maji yaliyotuama karibu na makazi ya watu au
hata ndani ya nyumba. Viluwiluwi vya mbu hawa huweza kuishi katika mazingara ya
ndani ya nyumba mpaka wakawa mbu kamili na kuanza kusambaza ugonjwa huu kwa
binadamu. Mbu hawa huwa na tabia ya kuuma wakati wa mchana.
Ugonjwa huu hauenezwi kutoka binadamu mmoja
kwenda kwa mwingine. Homa ya dengue inaweza kutibika kama
mgonjwa atapelekwa hospitali mapema na kupatiwa matibabu ya haraka. Hakuna
tiba maalumu ya ugonjwa wala chanjo bali mgonjwa anatibiwa kutokana na
dalili zitakazoambatana na ugonjwa huu kama vile homa, kupungukiwa maji au
damu. Endapo mgonjwa atachelewa kupatiwa matibabu, mgonjwa anaweza kupoteza
maisha.
Jinsi ya kujikinga na ugonjwa wa homa ya dengue
KUANGAMIZA MASALIA YA MBU:
- Fukia madimbwi ya maji yaliyotuama au nyunyuzia dawa ya kuua viluwiluwi vya mbu kwenye madimbwi hayo
- Ondoa vitu vyote vinavyoweza kuweka mazalio ya mbu kama vile, vifuu vya nazi, makopo, magurudumu ya magari yaliyotupwa hovyo, nk.
- Fyeka vichaka vilivyo karibu na makazi ya watu.
- Hakikisha maua yandayopandwa kwenye makopo au ndoo hayaruhusu maji kutuama.
- Funika mashimo ya maji taka kwa mfuniko imara.
- Safisha gata za paa la nyumba ili kutoruhusu maji kutuama.
KUJIKINGA NA KUUMWA NA MBU:
- Tumia dawa za kufukuza mbu “mosquito repellants”
- Vaa nguo ndefu kujikinga na kuumwa na mbu
- Tumia vyandarua vyenye viuatilifu (hata kwa wale wanaolala majira ya mchana)
- Weka nyavu kwenye madirisha na milango ya nyumba za kuishi
HATUA ZINAZOCHUKULIWA NA WIZARA YA AFYA:
- Kutoa taarifa ya tahadhari ya ugonjwa kwa Waganga Wakuu wote wa Mikoa na Wilaya kwa Tanzania Bara kupitia Makatibu Tawala na Wakurugenzi.
- Kuimarisha ufuatiliaji wa ugonjwa huu kupitia kwa Wataalamu wa Afya katika Mikoa, Wilaya na maeneo ya mipakani. Aidha uchunguzi wa ugonjwa huu utafanyika kwenye Mikoa na Wilaya zitakazoonekana kuwa na ongezeko la wagonjwa wenye homa.
- Kutuma vipeperushi vya ugonjwa huu katika maeneo ya mipakani ili iwapo msafiri anayeondoka au kurudi nchini akiwa na dalili tajwa atoe taarifa kwa watumishi wa afya wa mpakani ili hatua stahili ziweze kuchukuliwa.
- Kutoa mafunzo kwa watumishi wa afya na mipakani wa namna ya kutambua na kujikinga dhidi ya maambukizo ya ugonjwa huu pamoja na uchukuaji wa sampuli iwapo mgonjwa atapatikana.
- Kuanzishwa kwa vituo maalum vya ufuatiliaji wa ugonjwa huu katika hospitali 15 za mkoa wa Dar es salaam. Hospitali hizo ni pamoja na hospital ya Taifa Muhimbili, Hospitali zote 3 za manispaa ya Dar es salaam, kituo cha afya Kigamboni, Kituo cha afya cha Mbagala Rangi tatu, Dispensari ya Yombo Vituka, Kituo cha afya cha Mnazi mmoja, Dispensari ya Tabata A, Kituo cha afya cha Bochi, Kituo cha afya cha Mbweni, Hospital ya Mission Mikocheni, Hospitali ya TMJ, Hospital ya Regency na Hospital ya Hindu Mandal
- Kuimarisha Utambuzi wa ugonjwa katika maabara ili kuweza kuthibitisha ugonjwa huu
- Kufanya tathmini ya mazalio ya mbu ili kubaini ukubwa wa tatizo, jamii ya mbu wanaoambukiza ugonjwa, mazingira yao na jinsi ya kuwathibiti
HITIMISHO:
Wananchi wanashauriwa kutokuwa na hofu
kuhusu ugonjwa huu.
Ugonjwa huu si mpya. Mara ya kwanza kugundulika kuwepo kwa
ugonjwa huu nchini ilikuwa ni Juni 2010 mkoani Dar es salaam ambapo idadi
ya watu waliothibika kuwa na ugonjwa ilikuwa 40 na hakuna mgonjwa yeyote
aliyepoteza maisha.
Wananchi mnashauriwa kwenda katika vituo
vya tiba mara mnapoona dalili za ugonjwa huu.
Wizara inasisitiza kuwa hakuna vikwazo
vyovyote vilivyowekwa kwa ajili ya wasafiri wanaoingia na wanaotoka nchini. Wizara itaendelea kushirikiana na sekta
mbalimbali kufuatilia na kudhibiti ugonjwa huu.