Na Mwandishi Wetu, Moshi
Raia wa Pakistan, Kamran Ahmed anayetafutwa kwa udi na
uvumba na vyombo vya dola nchini, anadaiwa kuonekana akirandaranda katika mitaa
mbalimbali ya mji wa Moshi.
Raia huyo wa Pakistan anatafutwa kufuatia
amri ya kukamatwa kwake iliyotolewa na mahakama Machi 24 mwaka huu baada ya
mtuhumiwa huyo kutofika mahakamani bila taarifa yoyote.
Mshitakiwa huyo pamoja na watanzania
watatu, wanakabiliwa na mashitaka ya kusafirisha kinyume cha sheria, Wanyamapori
hai 152 wakiwamo Twiga wanne, kwenda Jiji la Doha nchini Qatar.
Twiga hao na wanyama wengine wenye
thamani ya Sh170.5 milioni, walitoroshwa kwenda Uarabuni Novemba 26,2010
kupitia uwanja wa ndege wa kimataifa wa Kilimanjaro (Kia).
Wanyama waliotoroshwa kwenda Doha
wenye thamani ya Dola 113,715 za Marekani sawa na Sh170.5 milioni za Tanzania,
walisafirishwa kwa kutumia ndege kubwa ya Jeshi la nchi ya Qatar.
Habari zilizopatikana jana zilieleza
kuwa pamoja na mtuhumiwa huyo kusakwa kwa udi na uvumba, lakini Jumamosi
iliyopita saa 6:00 mchana na juzi saa 2:20 usiku, alionekana katika mitaa ya
Moshi.
Kwa mujibu wa mtoa habari wetu,
Jumamosi alionekana akiwa katika gari aina ya Toyota Noah katika barabara ya
J.K Nyerere na juzi alionekana akitoka kununua mahitaji Rafiki Supermarket.
Kamanda wa Polisi mkoa wa
Kilimanjaro, Robert Boaz alipoulizwa jana, alisema wanazo taarifa za kutafutwa
kwake kutokana na amri hiyo ya mahakama lakini bado hawajafanikiwa kumpata.
“Tuna habari na jambo hilo
(kutafutwa) bado tunamtafuta,”alisema Boaz na alipoelezwa juu ya kuonekana
kwake, alishtushwa na taarifa hizo na kuwataka wenye taarifa sahihi kumpatia.
Hakimu Mkazi Mfawidhi wa mkoa wa
Kilimanjaro, Simon Kobelo anayesikiliza kesi hiyo alipoulizwa jana, alisema amri
ya mahakama iko pale pale na wenye wajibu wa kumtafuta ni polisi na wadhamini
wake.
Kesi hiyo imepangwa kusikilizwa kwa
siku mbili, Mei 6 na 7 mwaka huu na mahakama imeshatoa ilani ya kuwaita
wadhamini wake siku hiyo ili wajieleze kwanini wasichukuliwe hatua za kisheria.
Mbali na kesi hiyo, lakini
mshitakiwa Ahmed anakabiliwa na kesi nyingine ya uhujumu uchumi Jijini Arusha
ya kusafirisha ndege 80 kwenda Jiji la Guangzhou nchini China.
Katika kesi hiyo ya uhujumu uchumi
namba 27, Ahmed anatuhumiwa kati ya Januari 1,2005 na Septemba 14,2013
alisafirisha nyara za Serikali kwenda Guangzhou nchini China.
Ilidaiwa na mawakili wa Serikali
Elisaria Zakaria na Agustino Kombe katika kipindi hicho, mshitakiwa
alisafirisha kwenda China ndege 80 aina ya Pelican wenye thamani ya Dola 4,000
za Marekani.
Fedha hizo ni sawa Sh6.4 milioni za
Tanzania na kwamba kosa hilo ni kinyume cha kifungu namba 84(1) cha sheria
namba 5 ya uhifadhi wa Wanyamapori ya mwaka 2009.
Pia ilidaiwa kuwa katika kipindi hicho
hicho katika mikoa ya Dar Es salaam na Arusha, mshitakiwa aliwinda na kuua aina
saba ya Wanyama wenye thamani ya dola 28,520 za Marekani.
Wanyama hao na thamani yake kwenye
mabano ni Tembo (Dola 15,000), Chui (Dola 3,500), Duma (Dola 4,900),Nyati (Dola1,900),
Pofu (Dola 1,700), Pundamilia (Dola 1,200) na Swala (Dola 320).