MBUNGE wa Arumeru Mashariki, Joshua Nassari (CHADEMA), ameihoji
serikali ni kwanini isinunue mashine za kieletroniki (EFD) nchini China
ambako zinauzwa kwa bei ndogo.
Nassari amehoji hatua hiyo bungeni jana alipokuwa akiuliza swali la
nyongeza na kusema kuwa mashine hizo nchini China zinauzwa kati ya dola
50 hadi 100.
Akijibu swali hilo, Waziri wa Fedha, Saada Mkuya Salum, alisema
mashine zinazoagizwa na Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA), zina kiwango
na ubora na kwamba zina uwezo wa kutunza kumbukumbu.
Katika swali la msingi, Mbunge Viti Maalumu, Rita Kabati (CCM),
amehoji serikali kama haioni kuna umuhimu wa kutoa elimu ya kutosha kwa
walengwa kabla ya kuanza kutumia mashine zao.
Pia alitaka kujua ni kwanini serikali isiwe na mpango wa makusudi wa
kupunguza bei ya mashine hizo au kutoa ruzuku kwa kuzingatia malalamiko
ya wafanyabiashara.
“Mfumo wa kutumia mashine za Kieletroniki (EFD), ni mpya katika nchi
yetu na bado haujaeleweka vizuri kwa wafanyabiashara na ndiyo maana
kumekuwa na migomo ya wafanyabiashara kwenye baadhi ya maeneo nchini,”
alisema mbunge huyo.
Akijibu swali hilo, Naibu Waziri wa Fedha, Mwigulu Nchemba, alisema
mfumo wa kutumia mashine za kielektroniki za kutolea risiti (EFD),
ulianza rasmi nchini Julai mwaka 2010, umekuwa ukitekelezwa kwa awamu.
“Katika kuanzisha mfumo huu TRA ilianza kutoa elimu kwa
wafanyabiashara waliolengwa kutumia katika awamu ya kwanza ambao
walikuwa ni wafanyabiashara waliosajiliwa kulipa kodi ya Ongezeko la
Thamani (VAT).
Akizungumzia malalamiko ya wafanyabiashara kuhusu bei ya mashine
hizo, alisema serikali imeyafanyia kazi malalamiko hayo na kushusha bei
kutoka sh 600,000 na 800,000 za awali hadi kufikia kati ya sh 600,000
na 690,000 kulingana na aina ya mashine.