MBUNGE wa Kiembe Samaki, Waride Bakari Jabu (CCM) ameihoji serikali
ina utaratibu gani wa kuteketeza mbolea feki ambazo zimekuwa
zikiingizwa nchini.
Waride alitoa kauli hiyo bungeni jana alipokuwa akiuliza swali katika kipindi cha maswali na majibu.
“Katika miaka ya hivi karibu mbolea feki isiyokidhi viwango imekuwa
ikikamatwa kwenye maeneo mbalimbali nchini. Je, serikali ina mpango
gani wa kuikusanya na kuiteketeza mbolea hiyo, ili kulinda afya za
wananchi?” alihoji.
Akijibu swali hilo, Naibu Waziri wa Kilimo, Chakula na Ushirika,
Godfrey Zambi, alisema anakubaliana na mbunge huyo kuwepo kwa
changamoto kwa pembejeo zisizokidhi viwango na ubora katika soko.
Alisema serikali kupitia sheria ya mbolea namba 9 ya mwaka 2009,
ilianzisha Mamlaka ya Udhibiti wa Mbolea ili kuhakikisha mbolea
inayotumiwa na wakulima nchini inakuwa kwenye ubora unaotakiwa
kitaalamu.
Zambi alieleza mamlaka hiyo pamoja na mambo mengine, hufanya ukaguzi ili kuhakikisha kuwa mboleo ina ubora unaotakiwa.